Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Karoli Mwema, Mfiadini

Karoli Mwema, Mfiadini

Karoli alikuwa mwana wa Mtakatifu Kanuti mfalme mfiadini wa Denmark, alitawala nchi za Amiens (Ufaransa) na za Flandria (Ubelgiji). Karoli alistahili kuitwa "Mwema" kwa kuwa alikuwa mlinzi wa maskini. Alipolaumiwa kwamba anawapendelea mno maskini na kuwalaumu matajiri, alisema: "Hii ni kwa sababu najua sana shida za watu maskini na kiburi cha watu tajiri".

Mwaka 1125 kulitokea njaa kubwa sana. Kila siku mfalme Karoli aliwalisha maskini wapatao mia moja katika nyumba yake. Alikataza watu wasipike pombe ili nafaka itumike kwa kupika mikate. Akaamuru mbwa wote wauawe, kwa sababu walikuwa wanakula sehemu ya chakula. Akatoa amri pia watu walime ngano theluthi mbili ya mashamba na theluthi moja wapande mbaazi au maharage ambayo yanakua upesi. Alipogundua kuwa matajiri fulani walinunua vyakula na kuvilimbikiza kusudi wavilangue baadae, Mtakatifu Karoli aliwalazimisha kuviuza mara moja, tena kwa bei ya chini.

Jambo hili liliwakasirisha sana walanguzi hao hata wakamwua kanisani alimokuwa amekwenda na muguu mitupu kusali kama alivyozoea kufanya kila siku asubuhi.

Maoni


Ingia utoe maoni