Waanzilishi Saba Wa Shirika la Watumishi wa Bikira Maria
Mnamo mwaka 1233 kikundi cha vijana saba, waliojulikana kama vijana bora wa mji wa Florensi (Italia) walikwenda kuishi kitawa maisha ya upweke mlimani, siyo mbali na mji. Walitaka kujitenga na mambo ya ulimwengu, na kujitoa nafsi zao ili wawe watumishi wa Bikira Maria.
Palitokea shida maana watatu kati yao walikuwa hawajaoa, lakini wanne wengine walikuwa wameoa. Kati ya hawa wanne wawili walikuwa wajane. Walifanya mipango ili wale waliokuwa wakiwategemea wawaache katika hali bora ya maisha. Askofu wao alikubali mpango huo akawaruhusu wajitenge na ulimwengu na kuishi porini chini ya mlima. Walijenga kanisa la kawaida, wakaishi maisha magumu ajabu.
Basi, waliendelea kuishi hivyo miaka kadha mpaka siku moja wakatembelewa na Askofu wao na pia walipata ugeni wa Kardinali. Huyo alishangazwa na maisha yao, lakini aliwaonya neno moja: "Namna yenu ya kuishi inafanana mno na ile ya viumbe porini, kwa jinsi mnavyotunza miili yenu. Mnaonekana kama watu wanaotamani kufa zaidi kuliko kuishi, mpate uzima wa Milele. Fuateni mashauri ya wakuu wenu".
Maneno haya yaliwaingia sana moyoni watawa hawa saba; wakamwomba Askofu wao awape mwongozo wa maisha. Aliwaambia jambo kama hili linahitaji sala. Watawa walisali ili wapate mwanga na hapo Bikira Maria akawatokea. Mikononi mwake alikuwa na kanzu nyeusi na karibu yake alikuwapo Malaika ameshika kitambaa kimeandikwa jina 'Watumishi wa Maria'. Aliwaambia wafuate kanuni ya Mt. Augostino. Hivi walijulikana kwa jina la Watumishi Wa Maria, au Waserviti. Watumishi hawa wa Maria bado wanafanya kazi huko na huko duniani.
Askofu wao alitaka wapewe upadre, wakakubali na wakapewa. Lakini mmoja wao, Mt. Aleksis Falkonieri, kwa ajili ya unyenyekevu wake, akamwomba Askofu asimpe Upadre. Bradha huyu Aleksis aliishi maisha marefu kuliko wote. Inasemeka kuwa alikufa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Wanakumbukwa wote saba siku ya leo kwa sababu Mt. Aleksis alikufa tarehe ya leo, 17 Februari mwaka 1310
Maoni
Ingia utoe maoni