Porfiri
Porfiri alizaliwa Saloniki (Ugiriki). Alishika ufukara ambao Bwana Yesu anausifu katika Injili. Aliingia utawani jangwani, na huko alikaa muda wa miaka mitano. Halafu kusudi aweze kutembea pahali patakatifu, na pia kusali na kufunga, alikwenda uwandani karibu na mto Yordani (Israel). Alipokuwa na miaka arobaini, Askofu Mkuu wa Yerusalemu alimpa upadre, punde si punde alimpa uaskofu, atawale jimbo la Gaza (Israel). Kwa sababu ya mafundisho yake na miujiza yake, Mtakatifu Porfiri aliwaongoza watu wengi wakashika Imani ya kweli.
Mara kwa mara ilimbidi kukimbia sababu ya kuwakwepa makafiri waliotaka kumwua kwa sababu aliwakataza kuabudu sanamu za upuuzi. Pengine alijificha chumbani kwa kizee aliyekuwa na binti mdogo jina lake Irene. Basi, kizee huyu alimkaribisha vizuri na alimletea kila kitu cha kumfurahisha. Alimwambia kuwa hata yeye alitamani kuwa mkristu. Askofu alikubali, akaamuru afundishwe, na mwisho alibatizwa.
Irene alipokua, Askofu alimwuliza kama anataka kuolewa, akamwambia angemtafutia mchumba na kumpa mali pia. Lakini Irene alimjibu Askofu kuwa alikwisha mchagua Yesu Kristu awe mchumba wake, kwa hiyo hakutaka mwingine. Porfiri alimsifu Mungu kwa kuona jinsi nguvu ya neema inavyogeuza roho za watu. Irene alidumu katika ubikira wake mpaka kufa kwake, na wengine humheshimu kama Mtakatifu pamoja na Mt. Porfiri, ambaye alifariki mwaka 420.
Maoni
Ingia utoe maoni