Mwenyeheri Sebastiano Aparisio
Sebastiano alizaliwa Hispania kama mtoto wa wazazi maskini. Katika utoto wake kazi yake ya kawaida ilikuwa ni kuchunga Kondoo. Akiwa na umri wa miaka kumi na mitano, alipewa kazi nyumbani mwa mjane, lakini kwa sababu ya kushawishiwa naye tena na tena, akamwacha akawa mtumishi wa wakulima wenye mashamba makubwa. Alifanya kazi hii muda wa miaka mitano, na mshahara aliokuwa akiupata wakati huu, aliwapa wadogo zake waweze kulipia mahari na kufunga ndoa.
Baada ya hapo alivuka bahari ya Atlantiki, akaenda kukaa katika nchi ya Meksiko, Amerika ya kati. Kwanza alifanya kazi ya Utarishi, baadaye kazi ya kutengeneza barabara. Alifanya kazi kwa bidii sana, na kwa sababu alikuwa mtu mwenye akili, akatajirika kweli. Lakini alitoa fedha zake zote kwa sababu alizoea kuwasaidia maskini, pia kuwasaidia vijana kulipa mahari, na wakulima waliomba kukopa tu. Na Sebastiano hakuwaomba hata mara moja wamrudishie fedha hizo. Yeye mwenyewe aliishi kimaskini kweli.
Alipokuwa na umri wa miaka sitini alimwoa mwanamke maskini. Alipofiwa naye muda mfupi baadaye, akaoa mara ya pili. Alipofiwa tena, alikuwa na umri wa miaka sabini. Basi, aliwapa Waklara Fukara mali yake yote, akajiunga na Shirika la Wafransisko. Katika uzee wake akawa Mnovisi katika monasteri yenye watawa zaidi ya mia moja. Baada ya kuweka madhiri za utawa, aliishi bado miaka ishirini na sita. Muda huu wote alikuwa mwombaji akitafuta chakula kwa monasteri yake. Inasemekana kwamba uwezo wake juu ya wanyama ulikuwa wa ajabu: punda na hata wanyama wakali waliweza kutulizwa naye katika muda wa nusu dakika.
Katika miezi yake ya mwisho mzee Sebastiano alisikitika sana kutoweza kukominika kwa sababu ya kutapikatapika. Lakini Padre alimletea Sakramenti takatifu Chumbani mwake apate kuiabudu. Kuabudu, aliiabudu kwa raha kubwa na moyo wa ibada. Mwishowe akiwa na umri wa miaka tisini na nane, alimrudishia Mungu roho yake. Ilikuwa mwaka 1600. Mnamo mwaka 1787 alitangazwa rasmi kuwa Mwenyeheri.
Maoni
Ingia utoe maoni