Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Polikarpo

Polikarpo

Polikarpo alifundishwa dini na Mitume katika ujana wake akabatizwa. Alifanya urafiki na Mt. Inyasi wa Antiokia; na wote wawili walikuwa wafuasi wa Mtume Yohani. Mtume huyo ndiye aliyemfanya Polikarpo kuwa askofu wa Smirna (Uturuki). Askofu Polikarpo alipokuwa mzee alisafiri kwenda Roma (Italia) kuzungumza na Mtakatifu Papa Aniseto kuhusu maadhimisho ya Pasaka. Hatujui mambo mengi zaidi juu ya maisha yake, lakini Wakristu wake wa Smirna waliandika barua ndefu juu ya kifo chake kwa Wakristu wa Kanisa la Filomelium (Uturuki). Barua ile imetunzwa hadi leo, kwa njia hiyo tulipata habari kamili ya matukio.

Wakati ule Smirna ilikuwa chini ya serikali ya Roma, na zamani za Kaisari Marko Aurelio ilitoka amri iliyokataza Wakristu waliokuwamo katika milki ya Waroma wasifuate dini yao. Wakristu walikamatwa, na kwa sababu hawakukubali kuabudu sanamu ya Miungu ya uwongo, waliuawa. Polikarpo alichongewa. Walianza kumtafuta. Askari walimkuta amelala ghorofa ya juu katika nyumba ya mkulima karibu ya Smirna. Askofu angaliweza kukimbia lakini alikataa akisema: "Ni amri ya Mungu". Alishuka chini akawasalimu askari bila woga. Wao walipomwona kuwa ni Askofu mzee, tena mwenye mvi, zaidi ya hayo hakuwa na woga na aliwatazama kwa wema, walishangaa. Waliona haya kwa sababu ya kwa amri waliyopewa ya kumkamata na kumpeleka mahakamani. Aliwaomba ruhusa ya kusali kidogo. Kisha alimwambia mpishi wake awaandalie chakula. Aliwaacha wakila, akajitenga kidogo, akasali muda wa saa mbili.

Punda wake alipokwisha kutandikwa, Polikarpo alipanda, akafuatana na askari. Njiani walikutana na jemedari, jina lake Herodi, aliyekuwa akija kumkamata. Jemedari alimpandisha katika gari lake. Alianza kumwuliza maswali kwa upole, akijaribu kuyageuza mawazo yake. Jemedari alimwuliza Askofu Polikarpo: "Una shida gani? Hakuna dhambi kumwita Kaisari wangu mungu. Je, ni dhambi gani kutoa sadaka kwa miungu kwa ajili ya kujiokoa?" Alipoona Askofu hajibu neno, alizidi kumchokoza. Mwisho Mtakatifu Polikarpo alimjibu: "Sikia bwana, hakuna neno liwezalo kunigeuza, siogopi pingu wala upanga, mkuki, moto, maji wala teso liwalo lo lote lile. Siwezi kamwe kumfukizia ubani binadamu, sembuse, shetani". Majibu hayo yalimkasirisha jemedari yule. Alimshika Polikarpo akamsukuma, akamwangusha chini ya gari lake. Askofu mzee aliburutika njiani, na kuumizwa vibaya mguu mmoja.

Polikarpo alipelekwa barazani katika uwanja wa michezo. Liwali alimwuliza: "Ndiwe Polikarpo?" Askofu akajibu: "Naam". Liwali akamwamuru amwapize Kristu. Polikarpo alijibu: "Yapata Miaka thelathini sasa namtumikia Kristu, wala kwa muda huo wote hakunidhuru. Bali amenijalia neema nyingi. Ebu, fikiri mwenyewe kama naweza kumwapiza yule aliyenitendea mema matupu, aliyenisaidia, aliyenisimamia na kunitegemeza". Liwali alijaribu kumtisha akimwambia: "Usipoabudu ninavyokuamuru, utatupwa mbele ya wanyama wakali ili wakurarue". Polikarpo akasema: "Walete hao wanyama wakali, najua siwezi kujigeuza niwe mbaya zaidi, lakini naona bora niteswe, ili mateso yanitakase, yanifikishe uwinguni". Liwali alimwambia: "Huwaogopi wanyama? Basi, kama hugeuki sasa hivi, utaokwa". Polikarpo alinena: "Wataka kunitisha na moto? Moto ndiyo utakaozimika mwisho. Je, hujui moto ule uwakao milele? Utakaowaunguza wapagani? Nitese Upesi upendavyo".

Basi, zilikusanywa kuni, chungu nzima. Zilipokuwa tiyari kutiwa moto, Polikarpo alivua kanzu mwenyewe, akakataa kufungwa mikono kwenye nguzo, akinena: "Niacheni vivi hivi, mwenye kunipa moyo wa kuvumilia moto atanijalia nikae dhabiti, nisimame katika kuni pasipo kukazwa na viungo vyenu". Basi, alifungwa mikono nyuma, pasipokufungwa kwenye nguzo iliyokuwa imesimikwa kati ya lundo la kuni. Alipokwisha kupanda juu ya hilo lundo, aliinua macho juu, akanena: "Bwana wangu, Mungu Mwenyezi, ninakushukuru kwa sababu umenijalia siku hii na saa hii, niwe katika hesabu ya mashahidi wako, nionje nami bilauri ya Kristu nipate kuufikia uzima wa milele. Ninaomba nipokewe leo kati yao mbele yako, kama sadaka ya harufu nzuri. Ndivyo ulivyotaka, ndivyo ulivyoagua, ndivyo ulivyotimiza, ewe uliye Mungu kweli. Ninakushukuru, ninakutukuza kwa ulimi wa Kuhani wa Milele, anayekaa nawe Mbinguni, ndiye Yesu Kristu mwanao, mwenye kustahili sifa zote pamoja na wewe, pamoja na roho Mtakatifu, sasa na Milele, Amina."

Alipokwisha sema 'Amina' moto uliwashwa, lakini palitokea mwujiza mkuu: ndimi za moto hazikumteketeza, zilimwambaa zikamzunguka mfano wa tao. Wapagani waliokuja kumwangalia walipoona hawakufaulu kumwunguza, walimchoma upanga kifuani. Damu ilitoka kwa wingi, ikamwagika katika ndimi za moto, ikauzima, naye akafa. Alikufa shihidi namna hii huko Smirna katika uwanja wa michezo saa nane tarehe 23 ya mwezi Februari, mwaka 155.

Maoni


Ingia utoe maoni