Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Margarita wa Kartona

Margarita wa Kartona

Margarita alizaliwa Liviano, karibu na Kartona (Italia), mwaka 1249, akiwa mtoto wa mkulima maskini. Alipokuwa na umri wa miaka saba tu alifiwa na mama yake. Baba yake alimwoa mke wa pili ambaye hakumpenda Margarita, ndivyo sababu alipokuwa na miaka 18 aliondoka nyumbani kwenda kujitegemea. Uzuri wa mwili wake ukamponza. Kijana wa familia Sharifu alimchukua nyumbani mwake. Margarita alikaa naye miaka tisa. Hatujua kama walikusudia kuoana. Margarita alijipamba sana akafuata mambo ya anasa. Walipata mtoto mmoja.

Siku moja maisha haya ya raha yalitoweka. Kadiri ya mapokea mumewe alikuwa ameondoka kwenda kuwinda, akifuatana na mbwa wake. Baada ya siku mbili mbwa alirudi peke yake na kumlilia. Margarita alimfuata mbwa akakuta maiti ya mumewe msituni. Alikuwa ameuawa kikatili na maadui zake. Mwili wake umeanza kuoza na kutafunwa na wadudu. Margarita akashtuka sana, akafikiri rohoni mwake, hali yake yeye itakuwaje iwapo atakufa katika dhambi zake. Akasikitika akakimbilia kwa baba yake kumwomba toba. Alikata nywele zake, akajifunga kamba shingoni kama mtu aliyestahili kunyongwa, akawaonyesha wakristu wote kwamba anajuta kwa mwendo wake wa Uasherati.

Ndivyo Margarita alivyokuwa na vita kubwa rohoni kwa kushinda vishawishi vya shetani aliyemsumbua mno kusudi amrudishe katika maisha yake ya zamani. Lakini kwa kufunga na kusali, akapata kushinda, na Mungu akampa neema zake. Mwaka 1276, alikubaliwa kupewa vazi la Ndugu wa Toba wa Utawa wa Utatu wa Mt. Fransisko. Alihamia pamoja na mtoto wake katika nyumba huko Kortona ambako akaanza kuwasaidia akina mama waja wazito. Baadaye alianzisha hospitali, lakini mara nyingi alikwenda kukaa katika upweke kwa sala kwa muda fulani.

Mwisho, mwaka 1288, alihamia kabisa kwenye nyumba ya upweke mlimani. Katika miaka kumi ya mwisho wa maisha yake aliishi pale kama mtawa, akawa Mtakatifu mwenye kipaji maalum katika sala. Alifariki tarehe 22 Februari 1277. Papa alimwandika katika Orodha ya watakatifu mwaka 1728.

Maoni


Ingia utoe maoni