Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Petro Damiano

Petro Damiano

Petro Damiano alizaliwa Ravena (Italia) mwaka 1007. Wazazi wake walikufa alipokuwa angali bado mtoto, na yeye Petro Damiano aliishi nyumbani mwa mkubwa wake. Ndugu zake walimtendea vibaya, kama vile angekuwa mtumwa wao, wakampiga na kumtukana. Mwisho ndugu yake mwingine alimpokea kwake, akampa nafasi ya kusoma drasani.

Alipomaliza mafunzo yake alifundisha kwa muda mfupi, kisha aliacha ualimu na kuwa mtawa katika monasteri ya Makamalduli (wa Mt. Romualdi-tazama 10 Juni) hapo Fonte Avellana (Italia). Alichaguliwa kuwa mkuu wa watawa akajenga pia monasteri nyingine penginepo katika Italia. Alivutwa sana na mifano ya watawa wa zamani jangwani, na tabia yake ilifanana na tabia ya Mt. Jeronimo .

Katika matatizo ya siku zake aliwasaidia Mapapa wa Roma kwa maandishi yake juu ya teolojia na Sheria za Kanisa. Mwaka 1057 aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Ostia, na punde kidogo aliteuliwa kuwa Kardinali. Alikuwa wakili wao wa kuleta mabadiliko katika Kanisa. Alipokufa mwaka 1072 alianza kuheshimiwa mara moja kama Mtakatifu. Alitangazwa kuwa mwalimu wa kanisa, mwaka 1828.

Maoni


Ingia utoe maoni