Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Konradi

Konradi

Konradi alikaa mjini Plezansi (Italia). Kwanza alifuata anasa za dunia; furaha yake hasa ilikuwa kuwinda wanyama porini. Siku moja alipokuwa akiwinda, aliwaamuru wafuasi wake wachome miiba na majani walimojificha wanyama. Mara ukaanza kuvuma upepo mkubwa na moto ukaanza kuwaka kwa nguvu, hata ukaingia mashambani, ukateketeza mimea yote. Konradi alipoona hayo akaona hofu, akaondoka kimya hapo hapo. Mkulima mmoja akakamatwa, wakimdhania kuwa ndiye aliyewasha moto, akahukumiwa kunyongwa. Konradi alipopata habari akaenda barazani kuungama kosa lake kuwa ndiye aliyechoma moto. Hivyo alimwokoa mkulima huyo aliyeshtakiwa bure.

Konradi na mkewe walikuwa na shauri moja, wakuuza mali zao, nyumba, mashamba na wanyama, wapate kuwalipa watu waliopata hasara kwa mashamba yao. Kisha wakaamua kuachana, wakaenda kujivika mavazi ya kitawa: Konradi alijiunga na Wafransisko, mkewe akaingia katika konventi ya Mtakatifu Klara. Baadaye Konradi alikwenda kukaa katika kisiwa cha Sesilia akakaa pale miaka 40, na kazi yake ilikuwa kuwauguza wagonjwa wa hospitali. Usiku alilala katika pango la mlima, akafa huko huko mwaka 1351.

Maoni


Ingia utoe maoni