Teotoni
Teotoni alikuwa padre mwenye maisha matakatifu na hakuopenda raha za dunia. Alikuwa pia mhubiri hodari ambaye sifa zake zilienea mbali katika nchi ya Ureno. Aliwapenda sana maskini na roho za marehemu toharani, ambao aliwaombea kila Ijumaa kwa Misa za Wafu. Baada ya Misa, aliongoza maandamano kwenda makaburini na watu wote walimfuata.
Wakati ule Malkia wa Ureno alikuwa mjane, lakini alikuwa akitembea na mwanaume mmoja. Siku moja wote wawili walikuwepo kanisani wakati padre Teotoni alipohubiri kwa maneno makali. Ilionekana wazi yalikuwa yakiwaelekea wao. Waliona haya, na mawazo yao yakachafuka sana hivi kwamba wakatoka upesi kanisani. Safari nyingine Malkia huyo huyo alimpelekea ujumbe kabla ya kuanza Misa, akimwomba afupishe kidogo muda wa ibada. Padre Teotoni akampelekea Malkia ujumbe akisema kwamba alikuwa akitolea sadaka ya Misa kwa heshima ya Mfalme wa Mbinguni ambaye ni mkuu kuliko binadamu yeyote wa ukoo wa Kifalme hapa duniani. Akongeza kuwa Malkia ana uhuru kamili wa kukaa au kuondoka. Malkia alijawa na majuto, akangoja mpaka Ibada ilipokwisha, ndipo akaenda kumwomba radhi Mtakatifu na kupokea maonyo yake.
Padre Teotoni aliingia baadaye utawani, na huko akawa Abati. Aliishi humo miaka 30 ya mwisho ya maisha yake, akafa akiwa na umri wa miaka 80.
Maoni
Ingia utoe maoni