Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Walfrido

Walfrido

Walfrido alizaliwa Pisa (Italia). Alioa mwanamke aliyempenda sana, wakazaa watoto wa kiume watano na walau mmoja wa kike. Baadaye, Walfrido na mkewe Tesia walisikia moyoni kuwa Mungu anawaita waingie utawani. Walikuwa na marafiki wawili wenye ndoa ambao walikuwa na tamaa hiyo hiyo. Walikutana wakajadiliana juu ya maisha yao ya baadaye. Walichagua mlima mmoja wakajenga nyumba ya watawa wanaume. Kutoka hapo kwenda mwendo wa saa tano kwa miguu wakajenga konventi kwa ajili ya wanawake. Konventini humo humo wake zao na binti mmoja wa Walfrido wakavikwa shela ya utawa.

Utawa huu mpya uliwavutia wengi waingie, na baada ya kupita miaka michache idadi ya wamonaki iliongezeka kuwa sitini, kati yao akiwamo Gimfrido mtoto wa Walfrido. Gimfrido alifanywa kuwa padre, lakini alipata kishawishi kikubwa akatoroka utawani na watu wengine akachukua pia Farasi na hati zilizokuwa mali ya Jumuiya.

Walfrido aliona uchungu sana, akasali akimwomba Mungu amrudishe mwanae Gimfrido na kumpa alama itakayokuwa kumbukumbu yake maisha yake yote. Siku hiyo hiyo Gimfrido alikamatwa na kurudishwa utawani akiwa ametubu makosa yake. Lakini kidole chake cha mkono wake wa kuume kilikuwa kimeharibika vibaya sana hata hakuweza kukitumia tena.

Mtakatifu Walfrido alisimamia monasteri kwa hekima kwa miaka kumi, na alipokwisha kufa mwanae Gimfrido alirithi wadhifa wake, akawa padre mwema na mashuhuri.

Maoni


Ingia utoe maoni