Sirili & Metodi
Watakatifu Sirili na Metodi walizaliwa Tesalonike (Ugiriki) Mtakatifu Sirili alielimishwa huko Konstantinopoli (Uturuki), akawa mfilosofi wa sifa akasomesha katika Chuo Kikuu cha Kaisari. Metodi alikuwa ndugu yake, akawa mkuu wa mkoa. Wote wawili kisha kupewa Upadre walikwenda Moravia (Chekoslovakia) kuihubiri Imani ya Kikristu. Walitumwa na Kaisari wa Konstantinopoli kufanya hivyo. Walifaulu katika kazi hii. Wote wawili walifasiri sehemu ya Biblia na vitabu vya Ibada kwa lugha ya Kislavoniki, wakitumia herufi za Kisirili walizovumbua wao wenyewe. Mpaka wakati ule lugha ya Kislavoniki zilikuwa hazina maandishi ila zilikuwa zinasemwa tu. Lugha hii ya Kislavoniki bado inatumika siku hizi katika Liturjia ya Makanisa ya Wakristu mbali mbali katika nchi za Ulaya Mashariki na Urusi.
Baadaye waliitwa Roma, na huko Roma Mtakatifu Sirili aliaga dunia, tarehe 14 Februari mwaka 869. Metodi alifanywa kuwa Askofu, akaenda Pannonia (Hungaria). Huko hakuchoka kuhubiri Injili. Alikabiliwa na matatizo mengi, hasa alionewa wivu na watu ingawa alikuwa akisaidiwa na Papa. Alikufa Aprili 6 mwaka 885 katika nchi ya Chekoslovakia.
Baada ya kifo cha Mtakatifu Metodi wanafunzi wake walifukuzwa Moravia. Ndipo walipopata nafasi kueneza dini katika nchi ya Bulgaria na baadaye Ibada hizo zilienea pia Urusi. Kwa bahati mbaya uhusiano kati ya Kanisa la Roma na Makanisa ya Mashariki ulizidi kuwa mbaya. Mpaka Makanisa mengi ya Mashariki kujitenga na Kanisa la Roma katika karne ya kumi na moja baada ya Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni