Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Yosefu

Yosefu

Mtakatifu Yosefu, baba na Mlishi wa Yesu na Mume wa Bikira Maria, anasifiwa katika Maandiko Matakatifu kama "Mtu mwenye haki".

Yosefu alikuwa mtu mwenye moyo safi kabisa. Alichaguliwa kulinda Ubikira wa Maria, mama wa Mungu. Mafundi wa sanamu humchora Mt. Yosefu na ua jeupe mkononi kwa kutuonyesha uzuri wa roho yake aliyoilinda siku zote safi kabisa. Alikuwa mnyenyekevu kwa maana hakujivuna kwa sababu ya kuwa mwana wa ukoo wa mfalme Daudi, wala hakuchukia ilipompasa kufanya kazi yake ya useremala apate kuwalisha familia yake, na kumfundisha kijana Yesu. Tena alikuwa na mapendo makuu rohoni mwake kwa Yesu na Maria. Sasa anakaa Mbinguni karibu nao, tena anao uwezo mkubwa kwa Mungu.

Mtakatifu Teresia, aliyemheshimu sana Mtakatifu Yosefu, ametuambia: "Sikuomba kitu kwa baba mlishi wa Yesu nisikipate". Kama vile zamani Farao, mfalme wa Misri, alivyomweka Yosefu, mwana wa Yakobo, kuwa msimamizi wa milki yake, ndivyo sasa Mungu amemweka Mt. Yosefu kuwa msimamizi wa kanisa lake, akimwekea neema mikononi mwake, ili atugawie sisi tukimwomba kwa matumaini

Maoni


Ingia utoe maoni