Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Sirili wa Yerusalemu

Sirili wa Yerusalemu

Sirili alizaliwa Yerusalemu (Israeli), mwaka 315, na wazazi wakristu. Mt. Maksimo, askofu wa Yerusalemu, alimpa upadre, akaendelea kukaa Yerusalemu alimozaliwa. Kazi yake hasa ilikuwa kuwafundisha Wakatekumeni. Hakuacha lakini kuwatunza Wayahudi na Wapagani. Alijaribu kuwaongoa. Zamani hizo Wakatekumeni hawakuwa na ruhusa ya kuingia kanisani, bali walingoja mlangoni. Sirili aliwaendea akasimama kati yao, akawasomea na kuwaeleza neno la Mungu. Alizoea kuwaambia: "Msione haya sababu ya Msalaba wa Yesu Kristu. Pigeni ishara yake mwilini mwenu, katika pande la uso, mpate kuwapinga shetani wasioweza kuielekea bendera ya mfalme wenu. Pigeni ishara hiyo kila saa: iwe saa mnapokula au mnapokunywa, saa mnaposimama au mnapokaa, saa mnapofanya kazi, saa mnapotembea na saa mnapokwenda kulala, na saa mnapoamka. Msichoke kupiga ishara ya msalaba kila mara".

Sirili wa Yerusalemu anakumbukwa hasa kwa ajili ya masomo kumi na manane, aliyotoa wakati wa Kwaresma, kwa Wakatekumeni watakaobatizwa, na masomo matano kisha Pasaka juu ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi kwa waliobatizwa wakati wa Pasaka.

Mtakatifu Sirili alikuwa na huruma sana kwa watu maskini. Mwaka mmoja wa njaa aliviuza vyombo vya kanisa, apate kuwanunulia kande. Lakini maadui zake, yaani wafitini na wapinzani wa dini, wafuasi wa Arios, walimwonea wivu kwa ajili ya nguvu ya mafundisho yake. Walimchongea uwongo kwa serikali. Walimhamisha kwa nguvu za serikali, asipate ruhusa ya kurejea mjini mwake. Hata alipopata haki, alirudi Yerusalemu. Siku si nyingi baada yake, alihamishwa mara ya pili. Alirudi tena kisha kupata haki yake. Hata mara ya tatu alihamishwa, na alikaa ugenini miaka 10. Alirudi tena akaka Yerusalemu Miaka minane. Katika mafundisho yake alifumbua ukweli kuhusu dini ya Kikristu, wa Maandiko Matakatifu na mapokeo ya Kanisa pia, kwa moyo mkuu wa kiuchungaji. Alikufa mwaka 386. Alitangazwa kuwa mwalimu wa Kanisa mnamo mwaka 1883.

Maoni


Ingia utoe maoni