Patrisi
Patrisi alizaliwa na wazazi wa ukoo bora wa Kiroma. Alizaliwa huko Uingereza mwaka 385, baba yake alikuwa ofisa wa Serikali. Patrisi alipokuwa kijana bado alikamatwa na maharamia wakampeleka Ireland kuchunga mifugo. Kisha alitoroka akaenda Ufaransa kwa Mt. Germano, naye alimwongoza katika njia ya utakatifu kwa muda wa miaka ishirini. Baadaye alifanywa askofu, na akarudi Ireland. Kwa sababu alikuwa mtume hodari, dini ya Kikristu iliendelea sana Ireland na makanisa na monasteri nyingi zilijengwa. Wakristu hawakuogopa kuteswa sababu ya dini.
Patrisi alipenda kufa kama mfiadini. Mungu aliyekuwa na mipango mingine juu yake, alipenda aishi kwa muda wa miaka mingi hata akafa katika uzee. Siku moja alipokuwa akiwafundisha masista wa konveti ya Down, mara watu waliuona mwanga mweupe uking'aa makaburini. Walimwuliza Patrisi maana yake. Patrisi akageuka akamtazama Birgita, Mama Mkuu, akasema: "Haya mama, sema, mwanga huo maana yake nini?" Naye akajibu: "Mungu anatufumbulia ya kwamba hapo ndipo atakapozikwa mtumishi wake Patrisi". Patrisi alinyamaza, lakini alipowaaga masista, alimwambia Birgita asikawie kushona sanda yake. Alikwenda kwa Askofu mwanafunzi wake na ndipo akafa. Mama Mkuu, Birgita, alimfunika kwa sanda aliyoshona kwa mikono yake mwenyewe, na kaburi lake lilichimbwa pale pale palipoonyeshwa na Mungu mwenyewe kwa mwanga. Inasadikiwa kuwa Mt. Patrisi alifariki dunia mwaka 461, akazikwa huko Downpatrick (Ireland).
Maoni
Ingia utoe maoni