Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Teresia Margareta Redi

Teresia Margareta Redi

Teresia Margareta Redi alizaliwa Italia. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na minane, alijiunga na Shirika la Masista wa Karmeli. Alikaa katika utawa muda wa miaka mitano tu, wala hakuishi tofauti sana na Masista wenzake. Ndipo akiwa na umri wa miaka ishirini na mitatu, akafa.

Sista huyo alikuwa amejitoa kwa moyo Mtakatifu wa Yesu, na baada ya kufa kwake Masista wenzake walitambua wazi kwamba jambo hilo ndilo lililomfanya awe na huruma, hasa kwa wagonjwa. Ijapo alionekana kuwa mgonjwa yeye mwenyewe, hata hivyo, alikuwa daima mkunjufu na mvumilivu, akawa mfano wa mtawa anayejikamilisha na kupata utakatifu kwa njia ya kuongozwa na roho ya Shirika lake la kitawa, na kushika kiaminifu katiba yake.

Baada ya kifo chake, mwili wake haukuzikwa mara, bali uliachwa wazi muda wa siku kumi na tano wala haukuonyesha dalili yoyote ile ya kuharibika. Sala za wale waliyoomba msaada wa maombezi yake, zimesikilizwa mara nyingi sana, na hata miujiza mingi imefanyika kwa maombezi yake. Alitangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1934.

Maoni


Ingia utoe maoni