Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Toma wa Akwino

Toma wa Akwino

Mtakatifu Toma alizaliwa mwaka 1225 katika familia tajiri huko Akwino (Italia). Alisoma kwa Monte Kasino, halafu alikwenda Napoli. Toma alipopata umri wa miaka 19 aliingia Shirika la Mt. Dominiko. Wazazi wake walijaribu kumzuia, lakini yeye aliendelea kuwa imara.

Toma alipelekwa Koloni (Koln, Ujerumani) ambapo alifundishwa na Mt. Alberto Mkuu (Taz. 15 Novemba). Toma alikuwa mtu wa kimya asiyekuwa na tabia ya kudadisidadisi. Wanafunzi wenzake walimpa jina la "ng'ombe bubu". Siku moja aliulizwa neno gumu sana, alilijibu kwa akili hata watu wote waliokuwapo walishangaa. Mwalimu wake, Alberto Mkuu, alisema: "Bado kidogo mlio wa ng'ombe bubu huyu utavuma ulimwenguni kote". Toma aliondoka Koloni akaenda Paris (Ufaransa) kujifunza teolojia, akawa mwalimu mkuu.

Baadaye yeye mwenyewe alifundisha katika Vyuo Vikuu vya Paris, Roma na Napoli (Italia). Aliandika vitabu vya thamani kubwa. Wote wavisomao hushangazwa na elimu na akili bora ya Mt. Toma. Kwa kutaka kueneza katika kanisa lote Sikukuu ya Ekaristi, Papa aliwaita waalimu maarufu wawili, Toma na Bonevantura, watunge masomo, nyimbo, zaburi na sala. Basi, mapadre hao wawili waliandika hayo kila mmoja peke yake. Kisha waliitwa kwa Papa wamsomee waliyoandika. Baba Mtakatifu alishangaa rohoni kusikia uzuri wa masomo na nyimbo alizokuwa amezitunga Mt. Toma, kwa sikukuu ya Ekaristi. ' Sakramenti kubwa hiyo' ni moja ya nyimbo zilizotungwa na Mt. Toma.

Mt. Bonevantura (taz. 15 Julai) aliposikia Ofisio aliyotunga Mt. Toma, alilia machozi ya furaha. Pasipo kusema neno hata moja, alipasua karatasi aliyoandika Ofisio yake yeye mwenyewe, kwa maana Bonevantura aliungama bila kiburi kuwa Mt. Toma alimpita. Papa Urbano hakujua amsifu nani zaidi, Toma kwa akili yake, au Bonevantura kwa unyenyekevu wake.

Mt. Toma alikufa huko Fossanuova (Italia) tarehe 7 Machi, mwaka 1274, akatangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1323. Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 28 Januari kwa sababu siku hiyo mwaka 1369 mwili wake ulizikwa mara ya pili huko Tuluse (Ufaransa)

Maoni


Ingia utoe maoni