Eloji
Zamani zile, Magrebi, ndio Waislamu wa Moroko (Afrika ya Kaskazini), waliingia bara Hispania, wakakaa. Sultani wao alianza kuwasumbua na kuwadhulumu wakristu. Alitaka kuwaingiza kwa nguvu katika Uislamu. Wakristu wengi walifungwa gerezani na waliteswa sana.
Katika mji wa Kordova (Hispania), palikuwa na padre mtakatifu, jina lake Eloji, mtu mwenye elimu nyingi na bidii. Alikamatwa pamoja na askofu wake wakatiwa minyororo pamoja na Wakristu wengine, wakapelekwa gerezani. Walikaa siku nyingi kifungoni. Padre Eloji alikuwa nguvu yao. Hakuacha kamwe kuwaongoza na kuwatuliza. Kila siku aliwatia moyo na kuwasomea maandiko Matakatifu. Watu hawa hawakufanya woga, bali walikaa dhabiti mbele ya wadhulimu wao. Hata mwisho Waislamu hawakudhubutu kuwaua. Waliwafungulia wakawaacha waende zao.
Eloji alipokwisha toka gerezani alizidi kuwa na bidii ya dini. Aliwakaza moyo Wakristu wamuungame Yesu Kristu mbele ya Waislamu. Aliwaonya wasione haya kwa mambo ya Ibada. Kila mara lakini Wakristo walikamatwa wakauawa kwa sababu ya dini yao. Hata siku moja Sultani alipopanda darini juu ya nyumba yake, aliiona maiti ya wafiadini waliofungwa mikono nyuma kwenye nguzo karibu na soko. Hakuweza kuvumilia. Aliamuru maiti zifunguliwe, ziteketezwe katika tanuru la moto. Askari walipoanza kutimiza amri, mara Sultani alianguka chini asiweze kutamka neno, kwa kuwa ulimi wake ulipooza. Walimwinua, wakampeleka kitandani. Aliugua kutwa nzima, hata usiku, na kabla maiti za wafiadi hazijaisha kuteketea, alizimia roho. Mwanawe Muhamad akawa Sultani, akawa mkali kupita baba yake. Alitoa amri makadhi wazidi kuwatafuta Wakristu.
Askofu mkuu wa Toledo (Hispania) alipokufa, mapadre na wenyeji walimteua Eloji awe askofu wao. Ilikuwa mwaka 858. Lakini kabla wajumbe wao hawajafika Kordova kumwomba aende nao, alifungwa mara ya pili, hivyo hawakumpata kama askofu wao. Na sababu ya kufungwa kwake mara hiyo, ni kwamba alimpokea kwake Lukresia, binti mmoja wa kiislamu aliyekuwa ameiongokea dini Katoliki kwa msaada wa mkristu mmoja jamaa yake. Wazee wake Lukresia walimsumbua kila siku na kumshurutisha akane dini ya Yesu Kristu. Lakini Lukresia alikimbia na kuja kwa padre Eloji kupata shime. Eloji alimficha nyumbani kwa umbu lake. Waislamu walimgundua; basi, walimshtaki Padre Eloji kwa Kadhi.
Eloji alipoletwa barazani, kadhi alimwuliza: " Jinsi gani umemficha kwenu mwanamke wa Kiislamu?" Padre aliitikia: "Mtu ye yote ajaye kwetu kutaka kuelezwa dini, sisi mapadre hatuna budi kumpokea na kumfundisha dini, kwani ndio ujumbe tuliopewa. Ndiyo mambo yatupasayo kufanya katika dini yetu. Kadhi alipoona hatamweza, alitafuta vipengee, akamwambia: "Basi, mkane Yesu Kristu kwa midomo tuu mbele za watu wangu hawa. Tena ni hiari yako kushika imani yako ndani ya moyo wako. Ukikubali kufanya hivyo, nitakuacha. Utaweza kwenda zako ukawafundishe watu wako kama kwanza". Padre alilikataa shauri hilo kwa vile alilichukia mno. Kadhi hakuweza kuvumilia kukataa kwake. Alimkaripia akamwambia: "Nyamaza, au utakufa". Padre hakufadhaika kwa kitisho hicho. Alizidi kusema. Mwishowe alihukumiwa kukatwa kichwa.
Alipelekwa nje, hata alipokwisha fika kwa muuaji, alipiga magoti, akainua mikono juu, akafanya ishara ya msalaba na kusali, akijitoa sadaka, akiunga mateso yake na mateso aliyoyavumilia Bwana Yesu Msalabani. Kisha aliinama kichwa, akapigwa kwa upanga, akafa. Lukresia naye hakukubali kuikana dini, alikatwa kichwa siku nne baada ya kuuawa Mtakatifu Eloji.
Maoni
Ingia utoe maoni