Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Switberti

Switberti

Maisha ya Switberti ni kielelezo bora kuhusu matatizo katika maisha ya Wamisionari: matatizo ya usafiri katika nchi za misioni na vikwazo vilivyokuwepo kutokana na vita vya makabila ambayo wakati mwingine kuharibu ushindi wa mwanzo wa kueneza Injili.

Switberti ni mmojawapo wa kikundo cha Wamisionari kumi na wawili Waingereza na Wairishi walioongozwa na Mt. Wilibrodi. Wamisionari hao walitoka Uingereza mwaka 690, wakavuka bahari ya Kaskazini, wakaanza kueneza Injili kwa Wafrisi, kabila linaloishi Uholanzi na Ujerumani. Baadaye, walielekea upande wa kusini wakitembea umbali mrefu kwa nchi kavu wakifuata mto Rain. Hii ilikuwa shughuli kubwa sana kwa wakati ule. Walipata shida nyingi, na walivikabili vizuizi vingi, lakini mwishowe walifanikiwa, wakaanza kuhubiri na kufundisha katika sehemu zile. Mt. Switberti aliwaingiza watu wengi katika dini kwa utamu wa maneno yake.

Kwa sababu Wamisionari wenzake walimchagua kuwa askofu, Mt. Switberti aliamua kurudi Uingereza kutafuta Wamisionari wengi zaidi, na akiwa nyumbani alipewa daraja ya Uaskofu. Kabla ya kurudi Uingereza, alimwachia Mt. Wilibrodi kazi ya kuyaangalia makanisa aliyokuwa amekwisha kuyafungua.

Askofu Switberti aliporudi Ujerumani tena, baada ya kupewa Uaskofu, alipenya zaidi katika nchi na aliwabatiza watu wengi wa makabila mengine. Lakini kwa bahati mbaya sana, miaka michache baadaye Kabila la Wasaksoni waliteka na kuishikilia nchi, na hivyo kazi yake iliharibiwa vibaya sana.

Askofu Switberti alikimbilia katika kisiwa kimoja huko mto Rain na kujitayarisha kwa kifo chake. Alijenga nyumba ya kitawa na huko na alikufa hapo hapo kwenye nyumba hiyo, mwaka 713. Masalia yake yaliwekwa kwenye sanduku ambalo baadaye lilipotea. Lakini baada ya miaka 900 likapatikana tena. Bado linahifadhiwa na kuheshimiwa, na miujiza mingi imetokea kwa heshima yake.

Maoni


Ingia utoe maoni