Romano na Lupisini
Romano alizaliwa Ufaransa. Alipokuwa na umri wa miaka thelathini na mitano, alikwenda kukaa msituni katika mipaka ya Ufaransa na nchi ya Uswisi. Alichukua daftari alimoandikia maisha ya watawa watakatifu, na pia alichukua jembe, shoka na mbegu. Pale msituni alikaa chini ya mti mkubwa, akafanya kazi yake; kulima, kusali na kusoma maisha ya watakatifu.
Nduguye Mtakatifu Lupisini alikuwa na ndoa yake, lakini kwanza alifiwa na mke wake, halafu akafiwa na baba yake. Akawaza moyoni mwake, kufiwa vile na wazee wangu, ndiyo ishara Mungu hataki nikae zaidi katika dunia? Akaondoka, akamtafuta ndugu yake mkubwa Romano. Toka siku hiyo wakawa watu wawili kule utawani. Punde si punde watu walitaka kuyafuata maongozi yao, wakajenga nyumba za watawa.
Watawa hawa walikuwa wakifuata Sheria za Kasiano. Walilima mashamba, walifuga sana na hata hawakula nyama maisha yao yote. Mavazi yao yalikuwa ngozi za wanyama. Ngozi ikawafaa kwa mvua, lakini sio kwa baridi kali. Watu kutoka nchi zote za jirani walikuja kwa Romano na Lupisini kutaka msaada wa sala zao kwa sababu walikuwa wakiwaponya wagonjwa wengi.
Tumehadithiwa kuwa Mtakatifu Romano alifunga safari kwenda kusali kwenye kaburi la Mtakatifu Morisi. Basi, jua lilipotua, Mt. Romano alibisha hodi kwa watu maskini na wenye ukoma. Walimfungulia mlango mtawa huyu. Asubuhi walishangaa walipoona wamekwisha poma ukoma wao. Mt. Romano wakati ule alikuwa amekwisha kwenda zake. Lakini walimfuata, na wakampata njiani, wakamshukuru kwa furaha.
Mt. Romano alikufa mwaka 460. Mdogo wake Mt. Lupisini aliendelea kuishi utawani kwa miaka ishirini, akafa mwaka 480.
Maoni
Ingia utoe maoni