Gabrieli wa Maria wa Mateso
Fransisko Possenti alizaliwa Asizi (Italia) mwaka 1838. Alikuwa mtoto wa kumi na mmoja kati ya watoto kumi na watatu. Baba yake alikuwa mwanasheria mwadilifu, ambaye, alipochaguliwa kuwa mshauri mkuu mjini Spoleto, alihamia mji huo yeye pamoja na Familia yake. Mama yake Fransisko alikuwa na afya mbaya muda mrefu, alifariki dunia wakati Fransisko alipokuwa na umri wa miaka minne tu.
Kijana Fransisko alikuwa na tabia nzuri: mchangamfu, mcheshi na mkarimu, na hivyo akawa mtu mwenye kupendeka. Lakini alipokuwa amechukia au kukemewa, aliweza kukasirika upesi. Alikuwa na marafiki wengi, wavulana kwa wasichana; alipenda muziki na dansi, na kuvaa nguo maridadi. Wenzake walizoea kumtania wakimwita " Maridadi" na "Mcheza dansi". Aidha, alifurahia uwindaji na kupanda farasi, na kwa hivyo starehe za dunia zilimzuzua. Kwa jumla, alikuwa mtu wa kujipenda nafsi. Shuleni alijitahidi, na kwa vile alivyojaliwa vipaji vingi, aliyamudu vizuri masomo yake, hata akategemewa kuwa mtu maarufu baadaye, lakini hakuna kati ya walimu na wanafunzi wenzake aliyekuwa na wazo kwamba angeweza kuwa mtawa au padre baadaye.
Hata hivyo, dalili za wito zilionekana, na Fransisko alijishughulisha na mpango wa kujiunga na shirika la utawa kuliko walezi wake walivyojua. Mara mbili aliugua sana, na kila mara aliweka ahadi ya kuingia utawa kama angepona; lakini mara zote mbili, baada ya kupona, alisita kuitimiza ahadi yake. Alipofiwa na dada yake mpenzi Maria Luisa, akaamua mara kuwa mtawa, lakini kwa mara nyingine tena alisita. Basi, pole pole Fransisko alizidi kujihusisha tena na anasa za kidunia, akapanga urafiki na msichana mmoja, na wazee wa pande zote mbili waliufurahia na kuuchochea uhusiano huo. Hata hivyo, pengine Fransisko alijinyima muda wake wa starehe, akaenda kukaa mbele ya Ekaristi Takatifu na mbele ya sanamu ya Mama Maria. Lakini mwaka 1856 katika sherehe za Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, wakati wa maandamano sanamu ya Bikira ilipokuwa ikitembezwa mjini, ndipo Fransisko alipoguswa na neema za Mungu akisikia sauti dhamirini mwake: "Harakisha kuwa Mtawa!". Papo hapo ilikuwa kana kwamba miali ya mwanga ilimpenya mpaka ndani ya moyo wake wakati sanamu ilipokuwa ikipita mbele yake. Basi, safari hii hakusita zaidi, akamwomba ruhusa baba yake, akaingia katika Novisiati ya Watawa wa Mateso (au Wapasionisti) mnamo tarehe 10 Septemba mwaka huo huo, akapewa jina la kitawa Gabrieli wa Maria wa Mateso. Baada ya kuweka nadhiri za kwanza, akasomea upadre, lakini kamwe hakupewa upadre. Alipatwa na kifua kikuu na ugonjwa huo ulimdhoofisha sana. Hatimaye, aliaga dunia tarehe 27 Februari 1862, akiwa na umri wa miaka ishirini na minne.
Ingawa hakufanya mambo la ajabu, alipiga hatua kubwa katika maisha ya kiroho. Aliyatafakari sana mateso ya Yesu na Mama yake. Daima alikuwa mnyenyekevu na mtii, na aliwatumikia wenzake kwa kila namna. Uchangamfu wake ulikuwa furaha kwa wote, maongezi yake yalimpendeza kila mtu. Alikuwa mpole na mnyofu akichukia kila aina ya uongo na unafiki. Sifa ya miujiza iliyotokea katika kaburi lake, ilienea kwa haraka sana mara baada ya kifo chake. Gabrieli alitangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Benedikto XV mwaka 1920.
Maoni
Ingia utoe maoni