Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Leandri, Askofu

Leandri, Askofu

Leandri alikuwa Askofu wa Sevila (Hispania), mdogo wake, Mt. Isidori, alimfuata kama Askofu wa Sevila. Dada yake alikuwa ameolewa na mfalme wa Leovigildi ambaye alikuwa mfuasi wa uzushi wa Arios, na aliwafukuza wakatoliki. Hata alimtesa mwanawe Hermenigildi aliyeongoka na kushika dini ya Katoliki. Alimfunga gerezani na alimpeleka askofu mmoja mfuasi wa Arios kumpa Komunyo. Lakini Hermenigildi alikataa kabisa kupokea Komunyo hiyo kutoka kwa Mfuasi wa Arios. Hapo Leovigildi aliamuru askari wamchinje mwanawe gerezani.

Baadaye Leovigildi hakupata raha katika maisha yake, kwa sababu dhamira ya roho yake haikuacha kumkaripia ya kwamba amemwua mtoto wake. Alipokuwa karibu kuzimia roho alimwita Leandri, akamwomba amlee mwanawe Rekaredo. Leandri alikubali kwa furaha, punde si punde Askofu Leandri alifanya mtaguso katika mji wa Toledo (Hispania). Hapo wote waliuapiza uzushi wa Arios.

Kazi nyingine muhimu sana aliyoifanya Mt. Leandri ilikuwa kuibadili Liturjia ya Kihispania. Kwa kufuata mfano wa Makanisa ya Mashariki, aliamua Kanuni ya Nisea isemwe katika Misa ili kupinga uzushi wa Arios. Makanisa mengine ya magharibi yakafuata baadaye kanuni hiyo ya Ibada, na mwisho Roma yenyewe ikafuata mfano huo. Mt. Leandri alifariki Sevila, mwaka 600.

Maoni


Ingia utoe maoni