Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Skolastika

Skolastika

Skolastika alikuwa dada pacha wa Mt. Benedikto . Walizaliwa huko Norsia (Italia), mwaka 480. Wote wawili walijitolea kwa Mungu. Walipokufa walizikwa katika kaburi moja. Mtakatifu Benedikto alipojenga monasteri ya Monte Kasino, Skolastika alikuja kukaa karibu apate kufuata kanuni ya Wabenediktini.

Kila mwaka ndugu na umbuye walikuta katika nyumba moja, nje ya monasteri wapate kusimuliana mambo ya Mungu na furaha kubwa za mbingu. Walipokutana mara ya mwisho Skolastika alitamani sana kusikiliza mafundisho ya Benedikto, hata siku moja jua lilipoanza kutua alimsihi nduguye asiondoke. Lakini Benedikto alimgombeza akisema: "Haifai hata kidogo wamonaki kulala nje ya monasteri yao". Basi, Skolastika alianza kumwomba Mungu amzuie ndugu yake asiondoke. Alifunga mikono, aliinamisha kichwa chake mezani akasali kwa bidii, na kutoa machozi. Mungu alisikiliza maombi yake. Kwa ghafla yalikuja mawingu meusi na ngurumo ilisikika, na umeme ukametameta, na ghafla mvua ilianza kunyesha kwa nguvu sana. Benedikto alishindwa kabisa kuondoka akasema: "Mungu akusamehe, dada; je umefanya nini?" Skolastika akajibu: "Nilikuomba ubaki hapa, nawe ukakataa, nikamwomba Mungu naye akanikubalia". Wote wawili wakazungumza maneno ya Mungu usiku kucha.

Siku tatu baada ya hayo Benedikto aliona roho ya dada yake Skolastika ikipaa mbinguni mfano wa njiwa. Ilikuwa mwaka 547. Alimshukuru Mungu. Benedikto alitwaa maiti ya dada yake akaizika. Kisha siku arobaini Bebedikto naye alikufa, akazikwa humo humo katika kaburi la dada yake.

Maoni


Ingia utoe maoni