Jumapili. 24 Novemba. 2024

Mt. Apolonia, Bikira Mfiadini

Apolonia, Bikira Mfiadini

Zamani za Kaisari Filipo, Wakristu walifukuzwa vibaya katika Aleksandria (Misri). Wengi wao walikimbia kwa hofu kubwa walio kuwa nayo, lakini Apolonia alikaa akitamani kufa kwa ajili ya Yesu Kristu. Mt. Dionisi aliyekuwa Askofu wa Aleksandria wakati ule aliandika kwamba wapagani walimkamata Apolonia wakamfunga. Apolonia bila hofu yoyote, aliungama kwa uhodari dini yake. Alivumilia kwa saburi mateso yote watu wabaya hawa waliyomfanyia. Waliyang'oa meno yake, wakalivunja taya lake. Halafu walimpeleka karibu na moto mkali wakamtishia kumchoma angali mzima, lakini hata hivyo hakuikana dini yake. Apolonia alisimama kitambo akiwaza rohoni mwake, hatimaye, kwa uongozi wa Roho mtakatifu alijitupa mwenyewe kwenye moto. Watesi wake walipata aibu kubwa kwa kushindwa na huyu mwanamke hodari.

Wakristu humwomba Mt. Apolonia katika maumivu ya Meno, kwa maana Mtakatifu huyu aling'olewa meno kwa ajili ya dini yake.

Maoni


Ingia utoe maoni