Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Jeronimo Emiliano

Jeronimo Emiliano

Jeronimo Emiliano alizaliwa Vanis (Italia) mwaka 1486, akaingia uaskari alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitano, ili ajionyeshe kuwa shujaa kama babu yake. Siku moja alipokuwa akipigana vitani, alikamatwa na maadui, ambao walimtendea mabaya mengi, alidhulumiwa kwa kufungwa gerezani.

Inasemekana kwamba huko chumbani alilalamika akiomba msaada wa Mama wa Mungu. Alimwahidi Bikira Maria kwamba angeacha Uasherati wake na kutangaza kokote sifa za Maria ikiwa atajaliwa kuupata uhuru wake. Alipokwisha sali hivi, mara mwanga mweupe uling'aa. Bikira Maria alimtokea akiwa na Funguo za gereza mkononi. Alimfungua minyororo na hatimaye alimwamuru amfuate. Basi, Jeronimo alipita salama kati ya askari walinzi wa gereza.

Aliingia katika kanisa akaweka minyororo yake pamoja na funguo za gereza kwenye sanamu ya Bikira Maria, kisha akatundika godoro lake juu ya tao la kanisa. Baadaye, alieneza kwa watu wote sifa za Mama wa Mungu aliyemsaidia katika shida zake. Tangu siku ile Jeronimo aliukataa ukuu wa walimwengu apate kuwatunza maskini na wagonjwa. Alijenga nyumba za kuwapokea mayatima na wazee wasiokuwa na kwao.

Alianzisha pia shirika la mapadre wanaoendeleza kazi zake za kulea mayatima na kuwatunza wazee. Shirika hili liliitwa shirika la Mapadre wa Somaschi. Inasimuliwa kwamba Mtakatifu huyu alikuwa wa kwanza kuingiza desturi ya kufundisha dini ya Kikristu kwa watoto kwa kutumia Katekisimu yenye maswali na majibu. Alikufa huko Somaschi karibu na Bergamo akiwatunza wagonjwa wa tauni, mwaka 1537. Jina lake liliandikwa katika orodha ya Watakatifu mwaka 1767.

Maoni


Ingia utoe maoni