Yohane Bosco
Yohane Bosco (16 Agosti, 1815 – 31 Januari, 1888) alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mwanzilishi wa Shirika la Mt. Fransisko wa Sales. Alitumia maisha yake kuwaelimisha watoto na vijana wa mtaani, yatima na vijana wa magereza. Hakutaka kurekebisha vijana kwa ukali, bali kuwakinga dhidi ya maovu kwa wema. Upendo wake wa ajabu kwa vijana ndio siri ya mafanikio yake ya ajabu katika malezi.
Giovanni Bosco alizaliwa tarehe 16 Agosti 1815 akilelewa na mama yake mjane, baba yake alifariki mwaka 1917 akimuachia mke wake watoto watatu. Ilikuwa ni kipindi cha miaka migumu kutokana na maradhi na njaa, lakini mama yake alijitahidi kuwatunza na kuwalea vizuri.
Alipokuwa na miaka 9 Yohane alipata ndoto ya kinabii iliyomtabiria utume wake kwa vijana. Baadaye Mungu alizidi kumjalia karama nyingi za pekee.
Kufuatana na ndoto hiyo, Yohane aliamua kuwa padri, ingawa hakuweza kusoma hata shule ya msingi kutokana na umaskini wa nyumbani. Ndoto za kuwa Padri alizipata utotoni lakini kaka yake alimpinga vita na kutaka awe mkulima kama yeye. Lakini taratibu mama alimfanyia mpango dhidi ya upinzani wa kaka yake. Wakati huohuo alianza utume wake akitumia vipawa vyake vyaajabu. Alibahatika kukutana na Padri mzee ambaye alimsaidia katika kupata elimu kwenye seminari. Kwa shauri la Padri Yosefu Cafasso tarehe 30 Oktoba 1835 aliingia seminari ya Chieri. Tarehe 3 Novemba 1837 alianza masomo ya teolojia, na tarehe 29 Machi 1841 akapewa daraja takatifu ya ushemasi, na tarehe 5 Juni 1841 upadri huko Torino.
Katika kazi yake ya Upadre, pia alifundisha Katekisi kwa vijana, alitembelea wafungwa na kusaidia katika parokia mbali mbali nchini. Huko Torino kulikuwa na watoto 7184 chini ya umri wa miaka 10 waliofanya kazi viwandani. Yohane Bosco aliwatafuta ili kuwasaidia kijamii na kidini. Pamoja na Padri Cafasso alitembelea magereza akashtuka kuona hali ya wafungwa vijana. Kwa wema wake aliwavuta kumuahidia wamuendee mara baada ya kutoka. Muda mfupi baadaye vijana walikuwa wengi hivi hata akahitaji msaada wa mapadri watatu na vijana wakubwa kadhaa.
Hatimaye tarehe 12 Aprili 1846 alipata nafasi kwa vijana wake na kununua kibanda na kiwanja huko Valdocco. Mama yake pia aliamia katika kibanda hicho na wakasaidiana kutafuta na kuelea watoto yatima
Mwaka 1854 alianzisha shirika la mapadri kwa utume wa vijana (kifupisho chake ni SDB). Miaka 10 baadaye alianza ujenzi wa mahali patakatifu pa Bikira Maria - Msaada wa Wakristo (ndivyo alivyopendelea kumuita mama wa Yesu). Mwaka 1872, pamoja na Maria Domenica Mazzarello, alianzisha shirika la Mabinti wa Bikira Maria Msaidizi, ili walee wasichana kwa roho ileile.
Akiwa kama mwanzilishi wa Shirika la Mt. Fransisko wa Sales, mwaka 1875 alianza kutuma Wasalesiani wa kwanza huko Argentina, na wakati huohuo alianzisha kundi la watawa wasaidizi aliowaona kama Wasalesiani wa nje.
Yohane Bosco alifariki tarehe 31 Januari1888. Msiba wake ulihudhuria na maelfu ya watu. Mara baada ya kifo, jamii kubwa ilitamani zianze taratibu ya kumfanya Yohane Bosco kutambuliwa kama Mtakatifu
Papa Pius XI alimtangaza mwenye heri tarehe 2 Juni 1929 na mtakatifu tarehe 1 Aprili 1934 akipewa jina kama “Baba na Mwalimu wa Vijana. Sikukuu yake ni tarehe 31 Januari.
Maoni
Ingia utoe maoni