Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Gilberti

Gilberti

Gilberti alizaliwa Sempringhum (Uingereza), siku za mwisho za utawala wa mfalme Wiliam. Alikuwa mwana wa Joselini, ambaye alikuwa mkuu wa mji wa Sempringham. Joselini alimtuma Paris (Ufaransa) ili akasome huko. Akiwa Paris Gilberti alifuzu, na aliporudi alianzisha shule huko Sempringham. Aliwafundisha watoto wa watu maskini jinsi ya kupata utakatifu.

Punde baba yake alimpa urithi kutoka katika mashamba yake mawili huko Sempringham. Gilberti aligawa mali yake yote kwa maskini. Akivutiwa na fadhila zake, Askofu wa Lincon alimpa upadre ingawa Gilberti mwenyewe hakupenda sana. Baba yake alipokufa mwaka 1130, Gilberti aliondoka katika Jumba la askofu, akaanza kutumia urithi alioachiwa na baba yake. Alianzisha monasteri mbili peke yake. Moja ilikuwa ya masista waliofuata kanuni ya Wabenediktini, na nyingine ilikuwa ya wanaume waliojiita Wagilberti, wakafuata kanuni ya Mt. Augostino, nao walidumu mpaka wakati Mfalme Henriko wa Nane alipojitenga na Kanisa Katoliki. Wakati ule zilipatikana monasteri ishirini na sita za Wagilberti.

Mtakatifu Gilberti alipata taabu nyingi. Mabruda wake walimshitaki kwa Papa. Wakati mwingine alishitakiwa, ati, kwa kutoa msaada kwa Toma wa Becket (taz. 29 Desemba) aliyekuwa uhamishoni. Hii ilikuwa uongo, lakini kwa sababu hiyo alitupwa gerezani. Baadaye, aliupinga uongozi wa shirika lake hilo, na alifurahi kujiondoa na kuishi maisha ya kawaida ya jumuiya. Moja ya desturi zake ilikuwa kuweka mezani pake sahani aliyoiita 'Sahani ya Bwana Yesu', ambamo aliweka sehemu nzuri zaidi ya chakula kwa ajili ya maskini. Mtakatifu Gilberti alikufa mwaka 1190 akiwa na umri wa miaka 104. Alikuwa ameliomba shirika lake litoe misaada mingi kwa watu maskini na wenye ukoma. Alitangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1202.

Maoni


Ingia utoe maoni