Brigida, Mtawa
Baba wa Birgida alikuwa Mwairishi wa jamaa bora, jina lake Duptaku. Birgida hakuwa binti yake halali, maana alimzalia kwa mwanamke mmoja mtumwa. Baada ya kuzaliwa Birgida, yule baba alimfukuza kijakazi wake na mtoto huyo akabatizwa. Aliwekwa chini ya Ulinzi wa mama mmoja Mkristu ambaye aliombwa amlee Birgida kwa uangalifu katika uchaji wa Mungu na mapendo ya Ubikira. Baada ya miaka kadhaa Daptuka alipomwona binti yake anaendelea kukua kwa umri wa hekima, alimleta nyumbani kwake. Hapo Birgida alipendwa na wote kwa ajili ya fadhila zake za pekee kabisa zilizompamba rohoni na kuitia urembo tabia yake nzuri. Alikuwa msichana mnyenyekevu, mtulivu na mtii. Zaidi ya yote, mapendo yake kwa maskini yalikuwa ndiyo kiini cha tabia yake, hata alitafuta kila njia ya kuwasaidia.
Brigida alijitoa kabisa kwa Yesu, Mchumba wa mabikira, kwa nadhiri ya ubikira. Baba yake alimpa ruhusa kuingia utawani na kutimiza nia yake ya kuwa sista. Alikuwa na marafiki zake watatu wasichana ambao walimfuata huko utawani. Walijijengea vyumba vidogo, yapata maili ishirini kutoka Dublin (Ireland). Mahali hapa kulikuwa kitalu cha watakatifu, ndiyo asili ya monasteri nyingi katika Ireland.
Monasteri zote za huko humkiri Mtakatifu Birgida kuwa mama mwanzilishi wao. Sifa ya utakatifu wake na miujiza aliyokuwa akiitenda iliifanya Kildare itukuke sana. Hata wakati angali hai, watu walianza kujenga majumba mengi kando ya monasteri yake. Yalikuwa mengi sana hivi kwamba uliinukia kuwa mji mkubwa wa kutosha na kufanywa kuwa makao ya Askofu Mkuu wa Jimbo. Mtakatifu Birgida alifanya miujiza mingi, kati ya miujiza hiyo, mmojawapo ulikuwa ule wa kuwaponya wakoma wawili. Kwa sala zake alimfanya mwanamke mmoja kipofu kuona tena. Vile vile alimfanya msichana aliyekuwa bubu tangu kuzaliwa, aseme. Alimwinga shetani kwa watu wengi waliopagawa kwa kutumia alama ya msalaba tu.
Alikufa katika monasteri yake ya kwanza huko Ireland tarehe 1 Febuari 523. Maiti yake ilizikwa Kildare. Picha ya Mtakatifu Birgida pengine huchorwa akiwa amepiga magoti huku ameshika chombo chenye mdomo mpana; pengine huchorwa na ng'ombe karibu naye. Sababu yake ni kwamba siku moja Mtakatifu Birgida alifikiwa na wageni wengi, maaskofu bila kutarajia, wala hakuwa na chochote cha kuwaandalia. Alimlilia Mungu. Aliomba apate maziwa kwa kumkamua ng'ombe wake mmoja, mara tatu siku hiyo hiyo. Imani yake ilimponya. Aliweza kumkamua huyo ng'ombe maziwa mengi sana, hivi kwamba alikuwa sawa na ng'ombe bora watatu. Watu husali kwa Mtakatifu Birgida wanapokuwa na ng'ombe wagonjwa.
Maoni
Ingia utoe maoni