Yasinta, Mtawa
Habari za Mt. Yasinta zinashangaza sana kuliko masimulizi mengine kuhusu maisha ya Watakatifu. Ni jambo lisilo la kawaida kuona msichana ambaye amejitoa kabisa kuishi kikamilifu maisha ya utawa, aanze kuvunja kanuni waziwazi hata kuwakwaza watawa wenzake. Halafu anaongoka na kuanza kuishi vizuri kitawa, lakini baadaye anarudia maisha yake ya zamani. Mwishowe anapona udhaifu wake kwa kuitikia neema mpya ya Mungu na kukifikia kilele cha fadhila.
Klara Mariskoti alielimishwa katika konventi huko Italia, ambamo mmoja wa dada zake alikuwa ameshaingia. Inasemekana kuwa alionesha tamaa haba ya uchaji wa Mungu. Wakati dada yake mdogo alipofanyiwa mpango wa kuolewa, Klara alikasirika sana kuona wamemwacha yeye. Alionyesha hasira za waziwazi hata nduguze hawakuweza kumvumilia katika Familia. Matokeo yake kama ilivyokuwa desturi ya nyakati hizo, walimlazimisha kuingia utawani.
Basi, akawa mtawa na kuitwa Sista Yasinta, na baadaye akafunga nadhiri za maisha. Muda wa miaka kumi aliwakwaza masista wenzake kwa kuishi kama mtawa kwa nje, ndani lakini hakuwa na moyo wa kushika kanuni za kitawa. Siku moja alipokuwa mgonjwa, padre alikuja kumwungamisha chumbani mwake. Yule Padre alipoona jinsi alivyoishi kwa raha mstarehe, alimgombeza na kumwambia kuwa hii ni hatari kwa roho yake. Yasinta alionyesha dalili kuwa maonyo ya Padre yamemwingia, akaanza kugeuza mwenendo wake.
Lakini uongofu huu wa ghafla haukudumu muda mrefu. Alianza kurudi katika maisha yake mabaya ya kula raha. Ndipo Mungu akamletea ugonjwa mbaya zaidi. Tangu hapo akageuka kabisa, akaanza maisha ya kufanya Kitubio kwa kujitesa. Alilala muda mfupi na kusali muda wa saa nyingi.
Sista Yasinta akateuliwa kuwa mlezi wa Wanovisi, na aliwapa mwongozo wa kufaa watu wengi waliomwandikia barua za kumwomba mashauri yake. Yeye aliwaongoza watu wengi zaidi kwa Mungu kwa upendo wake kuliko wahubiri wengine wa nyakati zake. Alikufa tarehe 30 Januari, 1640, akiwa na umri wa miaka 55, na mwaka 1807 akatangazwa kuwa Mtakatifu.
Maoni
Ingia utoe maoni