Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Anjela wa Merichi

Anjela wa Merichi

Anjela alikuwa mtoto mpendelevu. Alizaliwa mwaka 1470 karibu na Breshia huko Italia. Alikuwa mtoto mcha Mungu tangu utoto wake. Alijitenga na watu ili apate nafasi ya kwenda kusali kanisani na dada yake. Alijitesa kisirisiri, alikula nusu tu ya chakula chake, aliondoka kitandani na kujilaza chini juu ya ubao mtupu. Furaha yake kuu ilikuwa kuwalea wasichana waliokuwa wakisumbiliwa na anasa za dunia. Daima alimwomba Mungu amwonyeshe njia ya kuishi vizuri duniani.

Siku moja alipokuwa akitembea shambani, alijitenga kando ili apate kusali. Mara aliona angani ngazi ndefu, akawaona mabikira wengi wakipanda ngazi hiyo wawili wawili, na malaika wakiwashikilia wasoanguke. Wakati huo sauti ilitoka juu ikinena: "Haya Anjela, uwe na moyo mkuu, kabla hujafa utalikusanya kundi la mabikira kama hawa".

Ilipopita miaka mingi ya kusali na kufanya kitubio, alianzishi Shirika la Mt. Ursula, mwaka 1535. Lilikuwa Shirika la kwanza la watawa wa kike wanaofundisha, wakamchagua Mt. Ursula kama msimamizi wao kwa sababu alikuwa wakati ule msimamizi wa vyuo vikuu na maendeleo ya wanawake. Masista wa Mt. Ursula husifika sana Ulaya kote kwa kazi yao ya kulea hasa wasichana fukara katika mwenendo bora wa Kikristu. Mt. Anjela alikufa mwaka 1540, akatangazwa kuwa Mtakaifu mwaka 1807.

Maoni


Ingia utoe maoni