Jumapili. 24 Novemba. 2024

Mt. Tito, Askofu

Tito, Askofu

Mt. Tito alizaliwa na wazazi wapagani. Aliongoka na kushika dini ya kweli, dini ya Kikristu. Paulo Mtakatifu alimchagua awe msaidizi wake katika kueneza Injili. Alimweka kuwa halifa wake, akawa askofu wa Kreta; naye Tito aliendesha kazi ya kitume aliyoianza Paulo kisiwani mle.

Mwaka 63 Mt. Tito alihubiri Injili katika nchi ya Dalmasia (Yugoslavia). Baadaye alirudi kisiwani mwake. Baada ya miaka mingi ya kazi bora alikufa kisiwani humo.

Alipokuwa bado hai, Askofu Mtakatifu huyu siku moja alipita mbele ya hekalu la Yupita, mungu wa uongo aliyeabudiwa sana na wapagani siku zile. Mara hasira takatifu ilimpanda, akaliapiza hekalu lile na jumba lote likabomoka palepale. Liwali Sekundo aliyekuwa amelijenga hekalu hilo kwa amri ya Kaisari allimjia Askofu, akamwomba amkinge na hasira ya Kaisari wa Roma.

Ndipo Mt. Tito alipomwamuru alijenge upya hekalu lile, lakini kwa heshima ya Mungu wa kweli. Liwali alifanya kama alivyoamriwa. Kanisa lilijengwa bila udhia kwa siku chache. Mwisho Liwali Sekundo aliomba abatizwe yeye mwenyewe na watoto wake.

Maoni


Ingia utoe maoni