Fransisko wa Sale
Mt. Fransisko alizaliwa katika mji wa Sale (Ufaransa), mwaka 1567.
Wazazi wake walimlea kitajiri kama ilivyokuwa hali yao. Lakini Mungu alikuwa akimvuta Fransisko rohoni, hata aliacha dunia akaingia upadre. Kwa kuwa alikuwa msemaji sana na mwenye kuwaka moto mtakatifu rohoni, alifaulu kuwaongoa Waprotestanti sabini elfu ambao walikuwa hawamo katika dini Katoliki. Upole wake usio na mfano uliwashinda wote, hata wakati roho yake ilipokuwa inataka kuwaka kwa hasira. Fransisko alijizuia siku zote. Aliweza kuvumilia kama kikondoo, matukano ya watu.
Baadaye alipofanywa Askofu wa Geneva (Uswisi) alistawisha sana jimbo lake. Alianzisha Shirika la Masista wa Maonano. Aliandika vitabu vyenye mafundisho mazuri juu ya kujiendeleza katika Utakatifu. Neno lake kuu lilikuwa: "Kufanya kila kitu kwa wema na upole".
Siku moja walimletea kijana mmoja mwanaume mwenye mwenendo mbaya wa uasherati ili amkanye, lakini kijana huyo alishupaa na hakumsikiliza. Hapo Mtakatifu huyu alimlilia na kumwambia atakufa vibaya. Na kweli, huyo kijana alikufa vibaya sana katika mapigano bila kutubu. Hakuzikwa na mtu, bali mbwa wa mwitu waliutafuna mwili wake. Hapo watu walimgombeza Mtakatifu Fransisko kwa sababu hakumkaripia kijana huyo mdhambi. Naye aliwajibu: "Nimefanya kazi miaka ishirini na miwili ili nifaulu, ingawa kidogo, kujipatia fadhila ya upole; mnadhani nitaipoteza kwa hasira ya mara moja? Ningefanana na mtu anayejaribu kumwokoa mwenzake asizame majini, huku mwenyewe anazama".
Mtakatifu Fransisko alikufa huko Lioni (Lyon, Ufaransa), tarehe 28 Desemba, mwaka 1622. Alizikwa huko Annes, Januari 24, 1623. Papa alimweka kama msimamizi wa waandishi, kwa sababu Mt. Fransisko aliandika vitabu vingi wakati alipokuwa akiwahubiria Waprotestanti.
Maoni
Ingia utoe maoni