Jumapili. 24 Novemba. 2024

Mt. Vinsenti Palloti

Vinsenti Palloti

Mt. Vinsenti alizaliwa Roma mwaka 1795. Alipokuwa mtoto hakuwaridhisha walimu wake. Siku moja mwalimu wake alisema: "Ni Mtakatifu mdogo, lakini ana akili nzito kidogo". Polepole akili zake ziliongezeka, akapewa upadre alipokuwa na umri wa miaka 23 tu. Baadaye alipata shahada katika teolojia na kuwa mwalimu msaidizi. Alitakiwa sana kwenda kuungamisha katika vyuo mbali mbali.

Alipokaa katika parokia fulani ambapo mapadre wenzake walimtesa ajabu, alivumilia mateso hayo muda wa miaka kumi bila kunung'unika. Kutokana na kazi bora alizofanya kwa watu, mwaka 1835 likatokea Shirika la Utume wa Kikatoliki ndio Mapadre na Mabruda Wapalotini. Lengo na karama zao ni kuunganisha juhudi za Wakristu katika kuchochea Imani na mapendo katika Kanisa na duniani kote.

Mt. Vinsenti Pallotti alianzisha shule za kufundisha dini na kusambaza vitabu vya dini. Alifungua pia shule za kufundisha kushona viatu, nguo, useremala, kilimo cha bustani ili vijana waweze kujiendeleza na kuona fahari ya kuweza kujitegemea.


Mara nyingi alirudi nyumbani nusu uchi kwa kuwa aliwagawia maskini nguo zake. Aliwapatanisha na Mungu wakosefu wengi. Safari moja alivaa kama mwanamke mzee ili aweze kukisogelea kitanda cha mtu ambaye alitishia na kudhamiria hasa kumpiga risasi padre yeyote wa kwanza atakayethubutu kumkaribia.

Mt. Vinsenti alikufa tarehe 22 Januari alipokuwa na umri wa miaka 55. Alitangazwa Mtakatifu mwaka 1963.

Maoni


Ingia utoe maoni