Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Anyesi (Agnes), Mfiadini

Anyesi (Agnes), Mfiadini

Anyesi alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili tu aliposukumwa mbele ya Altare ya Minerva aliyekuwa Mungu wa uwongo wakati ule mjini Roma (Italia). Akaamriwa kutii amri ya Kaisari na kutia ubani juu ya makaa ya moto kama ishara wazi ya kumheshimu mungu huyo. Bila ya hofu Inyesi alisimama mbele ya Altare kati ya askari na watesaji, akakataa kabisa. Akimwinulia Bwana Yesu, Mchumba wake, mikono, akafanya ishara ya msalaba. Pale pale akachukuliwa na kufungwa mikono na miguu, lakini mapingu ya chuma yalikuwa makubwa mno wala hayakuweza kuvifunga vifungo vyake vyembamba. Machozi yaliwalengalenga wapaganI walioshuhudia matukio hayo.

Basi, Anyesi alipelekwa mahali pa kuteswa, naye alikuwa radhi kabisa. Lakini hakimu alipoona kwamba wazo la kuumizwa na kuteswa halikumwogopesha Anyesi hata kidogo, wazo baya zaidi likamwingilia: Kumwumiza kwa kumwaibisha. Basi, Anyesi alivuliwa nguo kwa nguvu, akawa uchi mbele ya hakaiki ya wapagani. Hata hali hiyo haikumganya akubali kumwacha Yesu. Alisema: "Kristu huwalinda walio wake". Na, kweli, ndivyo ilivyokuwa. Kimiujiza Kristo alidhihirisha jinsi anavyothamini adabu njema ya macho. Msichana Anyesi alipoaibishwa na kuwa wazi mbele yao, wale wapagani wengi waliona haya, wakainama kichwa wasimwone. Lakini mvulana mmoja alithubutu kumtazama pasipo haya. Ghafla kimiujiza akapigwa machoni na kupofuka. Wenzake wakamchukua na kumpeleka mbali akilia sana, nusura kufa kwa maumivu na hofu kuu.

Hatimaye, uaminifu wa Anyesi kwa Kristu ulijaribiwa kwa ubembelezi na ahadi ya uchumba. Akajibu: "Kristu ndiye Mchumba wangu. Huyo alinichagua kwanza, nitakuwa wake". Basi, kisha hapo alihukumiwa kufa. Anyesi alisimama wima akisali, kisha akainama kichwa. Pigo moja tu la panga likatosha kumkata kichwa. Roho yake safi ikapelekwa juu kwa Mchumba wake Yesu.

Mtakatifu Anyesi hutajwa katika sala ya Ekaristi ya kwanza ya Misa Takatifu. Hivyo ni wazi heshima aliyokuwa nayo Kanisani tangu Zamani, na hata siku hizi yeye ni Mtakatifu apendwaye mahali pengi na watu wengi sana. Mtakatifu Anyesi huangaliwa kama msaidizi na mwombezi wa pekee mbinguni katika jambo la usafi wa moyo. Vijana wengi waweza saidiwa naye wakati mambo yashindanayo na fadhila hiyo, yanapozidi kuwasumbua kwa nguvu.

Maoni

John remigius

Naomba sala alizokuwa akizisali marakwamara au wanazozisari

Ingia utoe maoni