Margareta Burjwa
Margareta Burjwa (Bourgois) alizaliwa Ufaransa mwaka 1620. Alikuwa mtoto wa sita kati ya watoto 12. Alipokuwa na umri wa miaka 20, alitaka kuingia katika nyumba ya watawa, lakini hakufanikiwa, na hatujui kwa nini. Pengine alikatishwa tamaa, lakini alitulizwa na mtoto Yesu katika ndoto, ambapo alisema: "Jambo hili liliyapindua macho yangu kabisa kutoka kwenye uzuri wa dunia".
Mwaka 1652 Gavana fulani wa nchi ya Kanada alifika Ufaransa kutafuta mwalimu wa kike kwa ajili ya sehemu aliyokuwa anaishi. Margareta alikubali kwenda na alifika Kanada mwezi wa tisa mwaka 1653. Kwa miaka minne alitunza watoto, alisaidia katika hospitali, na kutayarisha kanisa dogo jipya. Mwaka uliofuata, shule ndogo huko Montreal ilifunguliwa ikiwa na watoto wavulana na wasichana.
Margareta alienda Ufaransa mwaka 1657 kupata wasaidizi zaidi, na baada ya mwaka mmoja alirudi na wanawake wanne. Alienda tena Ufaransa mwaka 1670, akapata wengine sita. Sasa akawa na uwezo wa kuanzisha Shirika la Watawa, lakini ulikuwa wakati wa njaa kubwa na matatizo mengi. Hata hivyo mwaka 1676 Shirika la Bibi Yetu lilikubaliwa na askofu wa kwanza wa Kanada. Baadaye, mwaka 1683, nyumba ya watawa iliteketezwa na moto. Masista wawili, akiwemo mpwa wake Margareta, walipoteza maisha yao.
Maaskofu wa Kanada hawakuzoea kuwaona masister wakifanya kazi nje ya nyumba yao ya kitawa, na ilichukua muda kabla mama Margareta hajaweza kuyakabili matatizo haya. Ilikuwa tu mwaka 1689 kwamba masista 24 waliweza kuweka nadhiri zao. Baada ya Miaka kadhaa Shirika limekuwa na nyumba za kitawa 200. Ashukuriwe Mama Margareta kwa bidii yake. Alipokuwa na umri wa miaka 79, alikufa tarehe 12 Januari, mwaka 1700. Alitajwa Mtakatifu mwaka 1950, na sikukuu yake ni tarehe 19 Januari.
Maoni
Ingia utoe maoni