Margareta wa Hungaria, Mtawa
Mt. Margareta alizaliwa mwaka 1242. Baba yake alikuwa Mfalme wa Hungaria, ambaye alijenga konventi kwa ajili ya Masista wa Shirika la Mt. Dominiko huko Budapest, mji mkuu wa Hungaria. Binti yake Margareta aliingia Konventi hiyo akiwa bado msichana. Alipoambiwa atoke kusudi aolewe na mfalme wa Bohemia, alikataa. Bila shaka angaliweza kuondolewa kizuizi cha kutoka utawani na kuolewa, pia baba yake Bela alionekana kupendelea jambo hilo kwa sababu ya kisiasa. Lakini Margareta alisema wazi kuwa alikuwa tayari kukatwa pua na mdomo wake kuliko kukubali kutoka utawani.
Alipokuwa anawahudumia wagonjwa wenye vidonda na majipu yenye kunuka vibaya, upendo wake kwa watu na upole wake uliwashangaza watu. Sista aliyefanya kazi kanisani alieleza ni jinsi gani Margareta alivyokuwa anamsihi aache wazi mlango wa kikanisa chao baada ya sala ya usiku, kusudi ashinde usiku kucha mbele ya sakramenti Takatifu badala ya kulala. Msichana aliyekuwa mtumishi wao alishuhudia kwamba: "Alikuwa mpole, mwema, mnyenyekevu kuliko sisi watumishi wa nyumbani".
Hapana shaka yoyote kwamba Margareta aliyafupisha maisha yake kwa kujitesa sana. Alikufa tarehe 8 Januari, mwaka 1270, akiwa na umri wa miaka 28 tu. Alitangazwa Mtakatifu mwaka 1943
Maoni
Ingia utoe maoni