Antoni wa Misri, Mkaa Pweke
Mtakatifu Antoni anajulikana kama mwanzilishi wa maisha ya kitawa. Hii ni kwa sababu alivikusanya vikundi vya Waeremita (Wakaa Pweke) vilivyotawanyika na kuvikusanya karibu karibu ili avisogeze, ingawa mwenyewe karibu muda wote wa maisha yake aliishi katika upweke.
Alizaliwa Misri mwaka 251. Baada ya kifo cha wazazi wake, ambao walikuwa wakristo hodari, Antoni alikwenda uwandani alipokuwa na umri wa miaka tisa kumtazama Mweremita mzee. Alijitenga na watu, akaishi upweke tangu mwaka 272. Hakuridhishwa na maisha ya uwandani kwa hiyo aliamua kwenda kukaa pangoni. Huko pangoni alisali na kumwomba Mungu. Mashetani walimwonea wivu, wakajaribu kumtisha kwa kuvaa sura za wanyama mbalimbali wakali. Walimfanyia makelele mengi na vitisho vya ajabu na hata kubomoa pango. Karibu Antoni angalizimia kwa mashambulio hayo, lakini alimtegemea Mungu. Alizoea kusema: "Mashetani huogopa kufunga, sala, uvumilivu na kazi nzuri".
Antoni aliendelea na maisha hayo mpaka mwaka 258. Alipokuwa na umri wa miaka thelathini na tano, alienda kushinda katika mahame katika mlima, ambapo aliishi maisha ya upweke karibu miaka ishirini bila kumwona mtu isipokuwa mmoja tu aliyemletea chakula kila baada ya miezi sita. Kwa sababu alisumbuliwa na wengine waliotaka kufuata mfano wake, alipokuwa na umri wa miaka hamsini na minne, alirudi kutoka mlimani na kuanza monasteri yake ya kwanza.
Aliwafundisha watawa wake kila asubuhi kwamba pengine wasingeweza kuishi mpaka usiku, na kila jioni kwamba ingewezekana wasiione asubuhi, tena aliwashauri kufanya kila tendo kama la mwisho katik maisha yao.
Katika mwaka 315 kulipokuwa na dhuluma kati ya Wakristu, Antoni alienda Aleksandria (Misri) ili kuwapa moyo watu waliokuwa wanateswa kwa ajili ya dini. Alivaa nguo yake nyeupe ya ngozi ya kondoo na kuonekana kama mtawala, lakini alikuwa mwangalifu asiwakasirishe waamuzi kama wengine walivyofanya bila kufikiri.
Maaskofu walimwomba arudi tena Aleksandria katika mwaka 335 kuwapinga wafitini wa Arios, akihubiri kwamba Mungu Mwana sio mtu tu, bali ni Mungu kama Baba. Alipoombwa na mtawala kukaa zaidi, Antoni alijibu: "Kama Samaki anavyokufa akitolewa kwenye maji, ndivyo mtawa anafifia akiacha maisha ya Upweke".
Mfalme Konstantino Mkuu alipomwandikia barua kuomba sala zake, watawa wengine walionyesha kushangaa. Lakini Mt. Antoni alisema: "Msishangae kwamba mfalme ametuandikia, hata hivyo mshangae kwamba Mungu ametuandikia, na kwamba ameongea na sisi kwa njia ya Mwanae".
Mt. Antoni alikufa tarehe 17 Januari, mwaka 356. Alikuwa na miaka mia moja na tano. Toka ujana wake alikaa katika hali ya kutokuwa na vitu viletavyo raha na anasa. Hata hakupata kuugua, aliona sawasawa, meno yake yalikuwa bado imara na hakuna hata jino moja lililong'olewa wala kulegea.
Maoni
Ingia utoe maoni