Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Inyasi wa Antiokia

Inyasi wa Antiokia

Mtakatifu Inyasi wa Antiokia
Askofu na Mfiadini


Inyasi huyo alikuwa mwanafunzi wa Mtakatifu Yohani Mwinjili. Katika uzee wake, akiwa askofu wa Antiokia (Siria), aliitwa aje mbele ya Mkuu wa mkoa naye akamwamuru kulikana hadharani jina la Bwana wetu. Askofu Inyasi akakataa kabisa, hapo basi licha ya uzee wake akahukumiwa auawe. Akapelekwa Roma (Italia) ili atupwe mbele ya wanyama wakali katika kiwanja cha michezo wakati wa michezo.


Katika safari yake, kwa meli, akilindwa na kundi la askari ambao mwenendo wao ulikuwa mbaya kadiri walivyotendewa vizuri zaidi. Ndivyo alivyoandika juu yao mzee askofu Inyasi. Katika safari hii ya kwenda Roma aliandika barua saba kwa makanisa, yaani majimbo, mbalimbali, nazo ni za thamani sana kwa kuwa katika barua hizo anaeleza juu ya imani ya wakristu wa karne ya kwanza, mwenendo wa kikristu, na muundo wa Kanisa wakati ule, yaani miaka kama sabini hivi baada ya Bwana wetu kupaa mbinguni.

Askofu Inyasi anasisitiza wasomaji wake walinde umoja kati yao na kukutana kati yao, ili chini ya usimamizi wa askofu wao waadhimishe Ekaristi. Katika barua aliyowaaandikia wakristu wa Roma, ili watangulie kuipata kabla yeye mwenyewe kufika, anawasihi wasijitahidi kumwombea uhuru. Barua hiyo inamdhihirisha askofu Inyasi kuwa mtu aliyempenda sana Yesu Kristu. hata asitake kuondolewa ile nafasi ya kumfia: "Mniruhusu kuyaiga mateso ya Mungu wangu". Ndivyo alivyowaandikia.

Wakafika mjini Roma ambapo wapagani walitamani sana kushuhudia kuuawa kwa watu wakati wa michezo; askofu Inyasi akatupwa mbele ya simba na kuliwa nao. Ilikuwa mwaka 107. Baadaye mifupa iliyobaki ikapelekwa Antiokia ambako toka karne ya nne, amekuwa akiheshimiwa kama mtakatifu.

Maoni

Emmanuel Mwanjila

Ahsante sana Kwa tafakari nzuri

Ingia utoe maoni