Jumamosi. 18 Mei. 2024

Mt. Hilari wa Pwatye

Hilari wa Pwatye

Hilari alizaliwa na wazazi matajiri wa Akwitania (Ufaransa) waliokuwa wapagani. Alipokuwa na umri wa miaka thelathini na mitano aliongoka na kuwa mkristu kwa kusoma Injili Takatifu. Hatimaye, aliteuliwa kuwa Askofu wa Pwatye (Poitiers, Ufaransa) mwaka 350. Katika hali yake hiyo alionekana kuwa Mtakatifu na mwenye elimu. Mt. Hilari ameandika vitabu bora vyenye mafundisho, hata nyimbo. Kitabu kilichosifiwa zaidi ni kitabu juu ya Utatu Mtakatifu.

Wafuasi wa mzushi Arios walimfukuzia uwandani mwa Frijia (Uturuki) alikokaa miaka minne. Mwishowe aliruhusiwa kurudi Ufaransa. Kabla ya kuingia Upadre, Hilari alipaswa kuwaaga mkewe na binti yake. Alitamani sana kumtolea Mungu binti yake. Alipokuwa ugenini alimwandikia barua nzuri sana akisema: " Mwanangu mpenzi, ningependa uwe binti mzuri mwenye heri. Ningependa uolewe na Bwana tajiri aliye na mali na almasi, apataye mali hiyo atatajirika kuliko watu wote duniani. Lakini kijana huyo hataki upokee pete wala mavazi ya kijana mwingine, uniambie kama wataka zawadi zake, halafu nitakutajia jina lake".

Apra (ndivyo alivyoitwa binti huyo) alitambua kuwa baba yake alitaka kumposa kwa Bwana wetu Yesu Kristu mwenyewe. Apra alimsihi baba yake amuombee kwa Mungu afe upesi ili amwone mchumba wake Yesu Kristu. Basi, Apra hakukawia kufa. Sasa yu katika kundi la mabikra wanaomfuata Yesu Mbinguni

Maoni


Ingia utoe maoni