Jumamosi. 18 Mei. 2024

Mt. Sesaria, Askofu

Sesaria, Askofu

Mt. Sesaria, Askofu wa Arle (Ufaransa), alikuwa Askofu hodari na mhubiri aliyesifika. Alihubiri kwa ufupi na kwa lugha ya kawaida kama inavyoonekana katika hotuba zake zilizopo hata leo.

Mnamo mwaka 512 alianzisha nyumba kubwa ya kukaa kwa wasichana wasioolewa pamoja na wajane. Na hii ilikuwa Konventi ya kwanza ya wanawake iliyopata kujulikana sana Ufaransa. Mt. Sesaria alitunga sheria za konventi hiyo. Moja ya kanuni izo ilikuwa kila mtawa ilibidi ajifunze kusoma na kuandika; na kanuni nyingine ni kwamba watawa peke yao wana haki ya kuchagua Mama Mkuu wao. Lakini kwa kuanzisha konventi hiyo ilimteua dada yake awe Mama Mkuu wa kwanza.

Baada ya muda mfupi konventi ikawa na watawa 200. Shughuli yao kubwa ilikuwa kuwalinda na kuwaelimisha vijana, kuwahudumia maskini na wagonjwa. Watawa hawa walishona nguo zao wenyewe, wakafuma na kuwashonea wengine nguo. Baadhi yao walifanya kazi ya kunakili vitabu, kwa kuwa uchapaji ulikuwa haujavumbuliwa bado. Watawa wote walijifunza muda wa saa mbili kila siku, na mmoja wao aliwasomea wenzake kwa muda fulani wakati wanapofanya kazi. Nyumba yao ilikuwa imefungwa kabisa siku zote, hakuruhusiwa mtu yeyote mwingine kuingia humo.

Askofu Sesaria alikufa mnamo mwaka 529.

Maoni


Ingia utoe maoni