Jumamosi. 18 Mei. 2024

Mt. Teodosi, Abati Mkuu

Teodosi, Abati Mkuu

Mt. Teodosi alizaliwa Kapodokia (Uturuki). Alipokuwa bado kijana alikwenda kuhiji nchi Takatifu. Alipofika huko akatamani kukaa upweke, ili apate kumtumikia Mungu. Basi, akakaa pangoni karibu na Betlehemu. Huko alisali kutwa kucha akimwaza Mungu.

Muda si muda akapata wanafunzi akawafunza uchaji wa Mungu. Baadaye, walipokuwa wamefikia kuwa kikundi kikubwa, wakajenga monasteri. Wagonjwa hata wazee wengi walikwenda kule. Mamonaki waliwatunza kama ndugu zao, wakiwapatia mahali pa kulala, na hayo wakayafanya kwa ajili ya mapendo ya Yesu Kristo.

Teodosi aliwakumbusha mamonaki wenzake ile amri ya kufa. Kwamba siku yoyote Mungu aweza kuwaita. Basi, kumbukumbu hiyo iweze kuwapo daima, akaamuru lichimbwe kaburi kubwa sana liwezalo kuwazika mamonaki wote hao. Kaburi lilipokuwa tiyari, akawakusanya mamonaki akawauliza: "Kaburi sasa tayari, nani wa kwanza atakayezikwa humo?". "Mimi”, akajibu monaki Basili. Basi, akapiga magoti akamwomba Teodosi ambariki. Sala za maziko zikafanyika kama desturi kwa mtu aliyekufa kweli. Kisha siku arobaini monaki huyo akafariki bila kuugua.

Mt. Teodosi akawekwa Abati Mkuu wa Mamonaki wote wa Palestina. Akakaa katika monasteri yake muda mrefu akimtumikia Mungu. Mwisho akafa mwenye umri wa miaka mia moja na tano.

Maoni


Ingia utoe maoni