Adriano
Adriano alikuwa Mwafrika kwa asili yake. Alipokuwa Abati wa monasteri moja karibu na Monte Kasino (Italia), mara mbili papa alimpa wadhifa wa kuwa Askofu Mkuu wa Kanterberi (Uingereza). Mtumishi huyu mnyenyekevu kwa Mungu alikataa kupokea wadhifa huu, lakini alimpendekeza monaki mmoja Mgiriki, Mt. Teodori ashike wadhifa huo badala yake. Papa alikubali, lakini alimkazia Adriano amsindikize Askofu mpya kwenda Uingereza.
Waliondoka kwenda huko mwaka 668, wakafika Kanterberi (Uingereza) wakati mbali mbali sababu ya matatizo ya usafiri. Baadaye kidogo, Adriano akatawazwa kuwa abati wa monasteri iliyoitwa baadaye Monasteri ya Mt. Augostino.
Alifundisha Kigiriki na Kilatini, Maandiko Matakatifu na hasa fadhila. Mtukufu Beda alisema kuwa wanafunzi walijifunza pia mashairi, elimu ya anga na kuhesabu kalenda. Baadhi ya wanafunzi walijua Kilatini na Kigiriki kama lugha yao ya Kiingereza. Mt. Adriano alifundisha muda wa miaka 39, akafariki dunia tarehe 9 Januari, mwaka 710. Akazikwa katika kanisa la monasteri yake.
Maoni
Ingia utoe maoni