Jumamosi. 18 Mei. 2024

Mt. Apolinari

Apolinari

Apolinari alikuwa Askofu wa Hierapolis katika nchi ya Frigia (Uturuki) naye huitwa "Mtetezi wa Dini". Alikuwa mwalimu mashuhuri kwa mafundisho yake ya dini ya Kikristu katika karne ya pili. Maandishi yake yalikuwa yakithaminiwa sana kwa ajili ya mafundisho yake bora na jinsi alivyoyaandika kwa ufasaha. Kwa bahati mbaya lakini mafundisho hayo yamekwisha potea.

Alijulikana sana kwa ajili ya utetezi wake wa dini ya Kikristu wakati alipomwandikia Kaisari Marko Aurelio mara tu baada ya kufanikiwa kulishinda kabila moja la Ujerumani kwa ajili ya sala za Wakristu. Kaisari huyo alikuwa amejaribu kwa muda mrefu kuwashinda Wajerumani kwa kutumia majemedari wake, lakini hakufaulu. Mwaka 174, aliamua kuliongoza jeshi lake yeye mwenyewe. Lakini jeshi lake lilizingirwa na wajerumani lisiweze kutoka, na wala halikuweza kuendelea kupigana kwa sababu katika eneo hilo hapakuwa na maji.

Kikosi cha 12 cha jeshi hilo kilikuwa na wanajeshi wengi sana wa Kikristu. Basi, jeshi lilipokuwa limejiandaa kwa mapigano, na askari wakiwa wamedhoofika kwa kiu, Wakristu walipiga magoti na kumwomba sana Mungu ili awape msaada. Ghafla, anga likawa jeusi kwa mawingu, na mara mvua ikaanza kunyesha kwa nguvu. Wakati huo huo Wajerumani walianza kuwashambulia. Waroma wakapigana huku wakinywa maji ya mvua waliyoyakinga katika kofia zao za chuma. Pengine walikunywa maji hayo yakiwa yamechanganyika na damu. Dhoruba iyoandamana na upepo mkali pamoja na radi na ngurumo, ilivuma dhidi ya maadui hao. Wajerumani hawakuweza kuona; wakaingiwa na hofu kubwa wakakimbia.

Mt. Apolinari huenda alikiandika kitabu kiitwacho UTETEZI (Apologia) akakituma kwa Kaisari mnamo mwaka 175 ili kumkumbusha fadhili aliyokuwa amepata kwa Mungu kwa ajili ya sala za Wakristu.

Maoni


Ingia utoe maoni