Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Raymundi wa Penyafort

Raymundi wa Penyafort

Raymundi alizaliwa mjini Penyafort mwaka 1175, wazazi wake walikuwa wa ukoo wa wafalme wa Aragoni (Hispania). Alipokuwa kijana bado alifundisha filosofia katika chuo cha Barselona (Hispania). Alijifunza pia sheria za Kanisa katika chuo cha Bolonya (Italia). Baadaye alipokuwa na umri wa miaka 47, aliingia shirika la Mt. Dominiko (taz. 8 Agosti). Alikuwa mhubiri hodari sana. Aliizungukia Hispania yote akifundisha watu.

Wakati ule sehemu kubwa ya Hispania ilikuwa inatawaliwa na Waarabu. Wakristu wengi walikuwa watumwa wa Waislamu hao. Maadili yao ya Kikristu yalikuwa yameharibika kutokana na kule kuwa watumwa kwa muda mrefu, na pia kutokana na uhusiano wao na Waislamu.

Mtakatifu Raymundi aliwaonyesha Wakristu jinsi ya maadui zao wa kisiasa. Walipaswa kuwashinda kwanza maadui zao wa kiroho na kuitiisha dhambi ndani yao wenyewe. Wakristu wengi waliolegea katika Imani yao, wakawa Imara tena. Kwa mashauri yake, Wakristu walipigana na Waislamu mpaka wakawashinda. Mt. Raymundi alikuwa akiheshimiwa sana na Mfalme Yakobo, hata hivi kwamba akamfanya kuwa mshauri wake.

Mnamo mwaka 1230, Papa alimwita Mt. Raymundi ili aende kukaa Roma (Italia), na akamwomba awe muungamishi wake. Ili kumpa malipizi ya dhambi zake, Mt. Raymundi alimwambia Papa apokee na kusikiliza maombi yaliyoletwa kwake na watu maskini na kuyatekekeza mara moja.

Papa naye alimwamuru Mt. Raymundi ayakusanye pamoja matangazo na maagizo ya Mapapa na ya Mitaguso. Baada ya miaka mitatu Mt. Raymundi akawa amemaliza shughuli hiyo. Akaandika vitabu vitano navyo tangu mwaka 1234 mpaka mwaka 1917 vilikuwa vinatumika kama sheria za Kanisa.

Mt. Raymundi alijishughulisha sana na kazi ya kuwaongoa Waislamu wa Hispania. Kwa lengo kama hilo hilo alimhimiza Mt. Toma wa Akwino (taz. 28 Januari) kuandika kitabu kiitwacho DHIDI YA WAPAGANI. Alianzisha nyumba za watawa kati ya Waislamu. Mnamo mwaka 1256 alimwandikia Mkuu wa Shirika lake kwamba Waislamu elfu kumi walikuwa wamebatizwa. Alikufa tarehe 6 Januari 1275, akiwa na umri wa miaka mia moja.

Maoni


Ingia utoe maoni