Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Teresia wa Mtoto Yesu

Teresia wa Mtoto Yesu

Teresia alizaliwa Ufaransa. Wazazi wake walipata watoto tisa. Teresia akiwa wa mwisho, kitindamimba. Wazazi waliwalea watoto wao katika uchaji wa Mungu. Wao wenyewe waliwafunza katekisimu, waliwasalisha sala za asubuhi na jioni, wakipiga magoti nyuma yao mbele ya msalaba uliotundikwa ukutani. Baba yao, akitoka nao matembezini, na ikiwa wanapitia mahali palipo na kanisa; basi huingia nao humo wakapeleka mbele ya altare ili wapige magoti na kuiabudu Sakramenti kuu. Njiani, walipokutana na maskini, baba alimwita Teresia, mdogo wao, na kumpa fedha ili ampelekee; mtoto humkimbilia yule maskini akamfumbatisha mkononi huku akimchekelea. Hivyo watoto hao walifundishwa upendo kwa Mungu, walivyoelekezwa kuyatekeleza matendo ya huruma. Miongoni mwa watoto wao, wasichana watano walijiunga na utawa.

Mtoto Teresia alikuwa mtundu sana, akiwa na tabia ya ukaidi na kiburi. Lakini mwaka hata mwaka akairekebisha tabia yake potovu, akainukia katika fadhila na bidii katika sala. Alipopata umri wa miaka mitano, mama yake aliaga dunia, Teresia akabaki mikononi mwa mpenzi baba yake na dada zake. Alipokuwa na umri wa miaka kumi, alipatwa na maradhi mabaya sana ambayo daktari hakuweza kuyatambua. Baada ya kuteswa na kwa muda mrefu, hatimaye, Bikira Maria akamponya kwa namna ya ajabu.

Alipokuwa angali mdogo, alijiunga na monasteri ya Wakarmeli huko Lisieu (Ufaransa), akadhihirisha, katika maisha yake, fadhila za upole, unyenyekevu, na imani thabiti kwa Mungu. Wakati huo, alikuwa amefikia umri wa miaka kumi na mitano. Kwa miaka tisa aliyombakia katika maisha yake mafupi, aliwafundisha wanafunzi wa utawa wake, kwa maneno na mifano yake. Huko utawani, hakutenda mambo ya ajabu; aliishi maisha ya kawaida tu, lakini alikuwa ameungana na Mungu katika kila tendo. Hiyo ndiyo aliyoiita "njia ndogo" yake.

Miaka miwili kabla ya kufa kwake, alipatwa na maradhi ya kifua kikuu, yaliyomletea mateso makali yakiandamana na kukohoa na kutema damu. Aliyatolea maisha yake kwa ajili ya wokovu wa watu, na unezaji wa imani katika nchi nyingine. Alifariki tarehe 30 Septemba, mwaka 1897, akiwa na umri wa miaka ishirini na minne. Katika mwaka 1925, alitajwa Mtakatifu, na Papa akamweka kuwa msimamizi wa misioni zote. Kabla ya kufa kwake, Mtakatifu Teresia alituhaidi kwamba atatusaidia kutoka huko mbinguni, na kweli tangu alipofariki, neema zilizopatikana kwa maombezi yake hazina idadi.

Maoni


Ingia utoe maoni