Baltazar, Kaspari na Melkiori
Epifania ni neno la Kigiriki, maana yake ni tokeo. Leo ni sikukuu ya Tokeo la Bwana. Mwana wa Mungu alipozaliwa kama mwanadamu kule Betlehemu, hakuna aliyejua habari zaidi ya Maria na Yosefu, mpaka Mungu mwenyewe alipojiweka kati na kuwatangazia watu wengine habari ya tukio hilo: kadri ya Injili ya Luka Mungu aliwatuma Malaika wawapashe habari wachungaji na kuwavutia waende kumwona mtoto aliyezaliwa; na kadri ya Injili ya Matayo aliwavutia wataalamu wa nyota waende Betlehemu kumwabudu mtoto aliyezaliwa Mfalme. Japo Injili haiyataji majina yao, lakini kutokana na mapokeo simulizi wamajimu hao wanaitwa Baltazari, Kaspari na Melkiori.
Hao walikuwa wataalamu wa nyota, na Mungu aliwaashiria kwa njia ya nyota ya ajabu. Kwa vile hao walikuwa si Wayahudi, sherehe ya leo hutufundisha kwamba Bwana wetu alizaliwa kwa ajili ya watu wote, wale walio Wayahudi kadhalika na wale wasio Wayahudi.
Wataalamu hao walimfahamu Mungu ambaye, kama asemavyo Paulo Mtume, aweza kujulikana kwa viumbe vyake kama jua, mwezi, sayari na nyota (Rom. 1: 19-20). Lakini ujuzi wao haukutosha, na Wayahudi wenye Maandiko Matakatifu walimfahamu vizuri zaidi. Hivyo wataalamu wa nyota tunaowakumbuka leo, walipofika Yerusalemu na kutokuiona tena ile nyota, walihitaji msaada wa Wayahudi, nao waliweza kuwasaidia kwa sababu maandiko Matakatifu husema wazi kwamba Bwana atazaliwa Betlehemu. Basi, wataalamu hao watatu waliweza kuendelea na safari yao kwenda Betlehemu baada ya kusaidiwa na Wayahudi.
Ajabu ni kwamba Wayahudi wenyewe, licha ya ujuzi wao kuhusu kuzaliwa kwa Masiha, hawakuenda Betlehemu. Walikuwa wametayarishwa na manabii muda wa karne nyingi kumpokea Masiha, lakini alipokuja, walibaki baridi tu.
Kujua tu habari ya Bwana hakutoshi. Wayahudi walikuwa na ujuzi, lakini hawakuutumia kimaisha. Wataalamu wa nyota yaani Baltazari, Kaspari na Melkiori, walikuwa na ujuzi kiasi kidogo tu; hata hivyo wakaiitikia nyota aliyowaonyesha Mungu, wakajitaidi kuongeza ujuzi wao kutoka kwa Wayahudi, na hivyo wakafika Betlehemu na kumwabudu Bwaba Yesu.
Maoni
Ingia utoe maoni