Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Mt. Simeoni wa Mnarani

Simeoni wa Mnarani

Mt. Simeoni wa Mnarani alikiwa mtoto wa Mchungaji maskini katika nchi ya Siria. Tangu utoto wake alipendelea kusali na kufunga. Alipopata umri wa miaka kumi na mitatu akaingia Monasteri. Baada ya muda kitambo, akaiacha monasteri hiyo apate kuingia nyingine ya watawa wale wenye kushika sheria ngumu zaidi. Akawazidi mamonaki wengine kwa ibada yake kuu, pasiwe na hata mtawa mmoja aliyefanana naye kwa fadhila ya mapendo kwa jirani na ile ya unyenyekevu.

Punde si punde akashauriwa na Padre Muungamizi wake aende kukaa uwandani chini ya kilima Telanisa. Hapo ndipo alipouanza mwendo wake Mtakatifu wa kushangaza akiongozwa na Roho Mtakatifu. Akala chakula kidogo tu, isitoshe ni chakula kilicho kibaya. Akautesa mwili wake usiku na mchana. Watu wengi sana, wakiona utakatifu wake, wakamwendea na kutaka shauri kwake. Simeoni hakupenda kabisa kusifiwa na watu. Basi, akajijengea mnara mdogo, ili ajitenge na watu akaishi juu yake. Kipenyo cha eneo hilo kilizidi kidogo tu mita moja u nusu, hivi kwamba hakuweza kujilaza kwa urahisi na kujinyoosha. Ili asianguke chini, aliuzungushia juu kwa ukingo.

Simeoni akaishi juu ya mnara kwa muda wa miaka arobaini hivi, akiwafundishawatu waliomjia, na akiwaombea kwa Mungu. Msidhani kuwa alifuata mwenendo huo wa ajabu kwa majivuno. La hasha! Bali, alijionyesha Mtakatifu wa kweli kwa kuvumilia kwa utulivu mateso yake na matukano ya wapotovu. Mungu mwenyewe akamtukuza mtumishi wake kwa kumjalia uwezo wa kutenda miujiza.

Shetani akamwonea wivu, akapata maadui wengi waliomcheka na kumdharau. Siku moja, watawa wenzake wakataka kumjaribu kuhusu utii wake, kuona kama atashuka chini, akiamriwa kufanya vile; wakamwambia: "Haya shuka mnarani, huishi kama binadamu wote". Mara Simeoni akaanza kushuka. Hapo wakatambua kama kweli yu mtakatifu wala si mnafiki tu. Akapata ruhusa ya kubaki juu ya mnara mpaka kufa kwake.

Maoni


Ingia utoe maoni