Elizabeti Ann Seton
Elizabeti alizaliwa mjini New York (Marekani) mwaka 1774 katika ukoo bora sana wa watu waliokuwa tajiri kweli. Baba yake alikuwa hana kawaida ya kusali; Mama yake, na baadaye mama yake wa kambo, walikuwa wote wawili waangilikani. Ndivyo alivyokuwa Elisabeti mwenyewe. Alifiwa na mama yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitatu tu, na baba yake alioa mara ya pili muda mfupi kisha hapo.
Akiwa na umri wa miaka kumi na tisa, Elisabeti aliolewa na William Seton, mfanyabiashara mwenye mali nyingi. Elisabeti alimzalia watoto watano. Matatizo na Ugonjwa viliwasumbua mara nyingi, lakini matatizo makubwa yalianza biashara aliyoifanya mumewe ilipopungua, na hata kufilisika, na mwenyewe akaugua kifua kikuu. Basi, waliamua kwenda Italia kutafuta matibabu yenye kumfaa, lakini hawakufanikiwa. Bwana Seton alifariki huko Italia, na Bi Seton alijiona kuwa mjane akiwa na umri wa miaka thelathini tu. Jambo baya zaidi lilikuwa kwamba alikuwa hana hela na huko watoto wake watano walimtegemea kabisa.
Wakati wa kukaa Italia pamoja na mume wake mgonjwa sana, Elisabeti alianza kugusana na dini katoliki, kwanza kidogo tu, alafu zaidi na zaidi. Tokea lake likawa kwamba mwezi Machi mwaka 1805 aliungama rasmi dini katoliki. Aliporudi nyumbani, Marekani, habari hiyo haikuwaridhisha ndugu zake hata kidogo, walimkasirikia kwa ajili ya kubadili dini yake, kiasi kwamba wengi sana wa marafiki na ndugu zake hawakutaka kushirikiana tena naye; wakamwacha kabisa, wala hawakumsaidia alipowaomba hela kwa ajili ya watoto wake.
Basi, ili aweze kuwapatia riziki na kuwalea vizuri watoto wake watano, Elisabeti alilazimika kufanya kitu. Kwa hiyo alianzisha shule mjini Boston (Marekani) mwaka 1808. Akina mama aliowavuta wawe walimu, walishirikiana kuishi kama kwamba ni watawa. Na hiyo ilikuwa hatua ya kwanza ya shirika jipya la watawa. Wakaruhusiwa kuweka nadhiri za watawa, na Elisabeti akawa mama mkuu wa shirika hilo.
Baadaye, aliwaambia masista wenzake hivi: "Lengo la kwanza la kazi yetu ya kila siku ninaloweka mbele yenu ni kutimiza mapenzi ya Mungu; la pili ni kuifanya kazi hii kama anavyotaka yeye; na la tatu ni kuifanya kwa sababu ni malenzi yake". Ndivyo mama Elisabeti alivyoanzisha shirika la kwanza la masista Wamarekani ambao walijiita "Masista wa Upendo". Alifungua shule nyingi za msingi na pia nyumba za mayatima, na -ikumbukwe-wakati huo huo aliendelea kuwatunza watoto wake watano.
Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka arobaini na sita tu, yaani mnamo tarehe 4 Januari 1821. Alitajwa kuwa Mtakatifu mwaka 1975.
Maoni
Ingia utoe maoni