Genoveva
Inasemekana kwamba, askofu katika safari zake za jimboni mwake, alikaa siku chache katika kijiji alimokuwa akiishi Genoveva. Wenyeji walipita mbele yake kumsalimu na kuomba baraka yake. Genoveva aliyekuwa mtoto wa miaka saba tu, alimwendea pamoja na wazazi wake. Hapo Askofu alimshauri Genoveva afuate wito wa Mungu akisikia moyoni mwake tamaa ya kuingia utawani. Genoveva alimjibu ya kwamba hiyo ndiyo iliyokuwa nia yake. Mwisho Askofu aliwaambia wazazi wake warudi tena asubuhi yake, pamoja na Genoveva.
Baba yake aliporudi na mtoto wake, Askofu alimwuliza Genoveva: "Je, unakumbuka unataka kufanya nini utakapokuwa mkubwa?" Genoveva akajibu: "Nakumbuka sana". Askofu akampatia Medali kuvaa shingoni, akamshauri asivae ushanga wala mapambo mengine. Basi, baadaye Genoveva aliendelea kama kawaida na kazi yake ya kuchunga ng'ombe.
Kisha kufa kwa wazazi wake Genoveva alihamia mjini Paris pamoja na mama yake wa Ubatizo. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na sita aliletwa mbele ya Askofu, akavikwa pamoja na wasichana wawili mavazi ya shela ya kitawa.
Siku hizo askari wa Atila walikuwa wakileta fujo katika nchi ya Ufaransa. Maaskari katili wengi sana waliushambulia mji wa Paris. Wakuu wa mji huo walitaka kuukimbia kwa hofu. Lakini Genoveva kwa maongozi ya Mungu, aliwakusanya wanawake wote wa mji huo, akawashauri wazidi kusali pamoja naye. Wanawake walifuata shauri lake, lakini wanaume walimtukana na kusema eti, alikuwa anaota ndoto tu, hata walitaka kumwulia mbali. Lakini punde si punde Atila na Askari zake walikwenda zao. Hapo ndipo watu wa Paris wakamshangilia Mtakatifu Genoveva kama mwokozi wao.
Katika maisha yake yote, Mtakatifu Genoveva alikuwa aliwatunza maskini na Wagonjwa. Mungu alimjalia hata uwezo wa kutenda miujiza kwa ajili yao. Mpaka hivi leo, watu wa Paris humwomba kama msimamizi wao.
Maoni
Ingia utoe maoni