Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Mt. Gregori wa Nazianze

Gregori wa Nazianze

Mt. Gregori alizaliwa Kapadokia (Uturuki) na wazazi bora wanaoheshimiwa na Kanisa kama watakatifu. Alizaliwa Karibu na Mji wa Nazianze mwaka 330. Alipokuwa mkubwa wa kutosha alipelekwa Atene (Ugiriki) akasome. Huko alikutana na Basili walifanya urafiki wa kusaidiana na kuendelea katika utakatifu. Kila jambo walilifanya pamaja, kuzungumza, kujifunza na kusali.

Walipomaliza masomo yao hapo Atene, Basili alikwenda zake ili apate kujitenga na malimwengu. Gregori alibaki papo hapo akifundisha lafudhi. Baba yake Mzee Gregori alipokuwa mtu wa Makamo alibatizwa pamoja na mke wake. Baadaye, alipata upadre na alikuwa askofu wa Nazianze kwa muda wa miaka 45. Alipokuwa na umri wa miaka 80, Askofu Mzee Gregori alimwita mtoto wake akamfanya padre ili amsaidie kulitawala Kanisa. Hatimaye, Gregori huyo mdogo aliwekwa kuwa askofu wa Nazianze. Aliwapinga kwa Uhodari wazushi wafuasi wa Arios.

Mji wa Konstantinopoli (Uturuki) ulikuwa ukishambuliwa pia na wazushi hao, na wakristo wengi walidanganywa. Wakuu wa Konstantinopoli walipoona vurugu hiyo, walimwita Gregori aje kuwaongoza. Kwa sababu ya uvumilivu na upole wake, Gregori alifanikiwa kutuliza hasira za watu, kuwafundisha; na kuwaongoza wazushi wengi katika dini ya kweli.

Baadaye ulitokea ugomvi kati ya wakuu wa Konstantinopoli. Gregori alijaribu kuwatuliza na kuwapatanisha, asiweze. Alipoona hawamsikii, alijiuzulu uaskofu wa Konstantinopoli akaenda kukaa Nazianze. Alikufa mwaka 390. Maiti yake ilihamishiwa Roma, na sasa hivi Kaburi lake limo katika Kanisa la Mt. Petri huko Roma.

Maoni


Ingia utoe maoni