Gaspari de Bufalo
Mt. Gaspari ni Mwanzilishi wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu. Alizaliwa Roma mwaka 1786, akapewa upadre mwaka 1808. Muda mfupi baadaye Roma ilitekwa na Jeshi la Napoleon, Kaisari wa Ufaransa. Padre Gaspari pamoja na mapadre karibu wote wa Roma walipelekwa uhamishoni kwa sababu walikataa amri ya Kaisari Napoleon ya kutomtii Papa. Alirudi Roma baada ya kuvunjika kwa utawala wa Kaisari Napoleon. Huko alikuta shughuli nyingi zikimngoja sababu kwa muda wa miaka karibu mitano Roma haikuwa na Mapadre wa kutoa Sakramenti.
Alianza kazi za kimisionari na kuanzisha Shirika la Damu Takatifu ya Yesu. Lengo na karama za Shirika hili ni kuwahudumia waasi wa dini na walegevu ili wamrudie tena Mungu. Mapadre na Mabruda wote hushirikiana katika kulistawisha neno la Mungu mioyoni mwa vikundi vya vijana, wakulima, walimu na wafanyakazi. Kwa hiyo wanashirika hujiandaa kwa shughuli hizo kwa njia ya sala, elimu na kazi.
Jambo moja, kati ya mawazo yake, alilolitilia mkazo ni kwamba kila mtu anapaswa kufanya kazi. Ndiyo maana alianzisha mjini Roma kazi za huduma ya upendo kwa ajili ya vijana na wazee, matajiri na maskini, waume kwa wake.
Mbinu za kimisionari za Mt. Gaspari zilikuwa za ajabu na za kusisimua sana. Inasemekana hotuba zake zilikuwa mithili ya tetemeko la roho. Kila alipomaliza mahubiri ya mafungo kwa watu, zana za vita zilizokatazwa, vitabu vilivyisimulia mambo ya zinaa, na kitu chochote ambacho kingeweza kumchukiza Mungu, vilichomwa moto hadharani. Mahali pale pale vilipochomwa moto vitu hivyo, ulisimikwa msalaba kama kumbukumbu, na wimbo wa kumshukuru Mungu uliimbwa. Kisha Wamisionari walitawanyika kimya kimya.
Mahubiri yake ya mwisho ya mafungo kwa waumini aliyatoa Roma wakati Ugonjwa wa kipindupindu ulipozuka mwaka 1836. Alikufa mwaka huo huo Roma, na mwaka 1954 alitangazwa kuwa Mtakatifu.
Maoni
Ingia utoe maoni